Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaushukuru Umoja wa Mataifa na Jeshi la Tanzania kwa kuzingatia usawa wa kijinsia

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, katika kikosi cha tano, TANBATT-5 kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaolinda amani nchini Mali, MINUSCA, akimsaidia mwanamke kubeba maji.
Meja Asia Hussein/TANBATT-5
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, katika kikosi cha tano, TANBATT-5 kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaolinda amani nchini Mali, MINUSCA, akimsaidia mwanamke kubeba maji.

Tunaushukuru Umoja wa Mataifa na Jeshi la Tanzania kwa kuzingatia usawa wa kijinsia

Wanawake

Tukiwa bado tuko katika mwezi wa wanawake ambao umekuwa na matukio kadhaa makubwa kama maadhimisho ya siku ya kimataifa ya wanawake duniani na siku ya majaji wanawake, wanawake wanajeshi walinda amani kutoka Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha 5 kutoka Tanzania kinacholinda amani kupitia mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCAR, wameushukuru Umoja wa Mataifa pamoja na Jeshi lao la Tanzania kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika mipango ya ulinzi wa amani.

“Nimeipokea fursa hii kwa mikono miwili kwani katika kundi kubwa la wanaume na wanawake tupo. Inaonesha kwamba, sisi wanawake tunaweza kufanya kazi sawa na wanaume.”  Ni maneno ya  Sajenti Asha Idd Mwanamdoe mmoja wa walinda amani wa kutumaini katika TANBATT 5 ambaye ameanza kwa kueleza namna alivyoipokea fursaa ya kuhudumu katika kikosi cha 5 cha Tanzania cha kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na kisha  anaendelea akitofautisha na hali ilivyokuwa katika siku za nyuma akisema, hali tofauti na huko awali siku za nyuma ilikuwa ikionekana kwamba wanawake hawawezi kufanya kazi sawa na wanaume ila kwa sasa imeonekana kwamba "sisi tunaweza kufanya kazi sambamba kabisa na wanaume. Na nitaitumikia nafasi hii kwa ufanisi na kwa weledi mkubwa katika kutekeleza yale yote maagizo yaliyotolewa kwa majukumu ya kazi.” 
 
Mwingine ni Sajenti Abeda Juma Mtwana, yeye pamoja na majukumu mengine, anashughulika na ukalimani ili kuwezesha mawasiliano. Ueledi wake katika lugha ya kifaransa unasaidia kuhakikisha wanawake wa CAR wanasikilizwa kama anavyoeleza akisema, "inatupa urahisi au wepesi kuweza kuchukua matatizo au kero zinazowakabili wanawake wenzetu zinapitia kwangu moja kwa moja tofauti na kupitia kwa wanaume inakuwa haipendezi. Kwa hiyo kupitia fursa hii mimi ninawezesha kuchukua zile changamoto na kuzipeleka sehemu husika kwa ajili ya utatuzi.” 
Wananchi wa CAR wakifurahia kupokea maji kutoka kwa Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha tano, TANBATT-5 chini ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaolinda amani nchini Mali, MINUSCA.
Meja Asia Hussein
Wananchi wa CAR wakifurahia kupokea maji kutoka kwa Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania wanaohudumu katika kikosi cha tano, TANBATT-5 chini ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaolinda amani nchini Mali, MINUSCA.
 

Mwingine ni Staff Sajenti Martha Cosmas Julius, yeye analenga kuitumia nafasi hii kubadilisha fikira za jamii kwa kuanzia na wanawake wenyewe ili lengo namba 5 la Malengo ya Maendeleo Endelevu kuhusu Usawa wa Kijinsia litimie huku akitoa ahadi kwamba  kwa nafasi yake kama mlinda amani mwanamke, atajitahidi sana kuwaelimisha wanawake wenzake, "kwamba mwanamke anaweza kupata au kusababisha maendeleo yakapatikana. Kinachotakiwa ni kwamba hatakiwi mwanamke au wanawake hatutakiwi kuangalia ni changamoto gani ambazo zinajitokeza au tunazozipitia kikubwa ni kusonga mbele kwa lengo la kupata maendeleo au kufanikisha maendeleo katika jamii na ninachoamini ni kwamba penye mafanikio au penye maendeleo pana sauti na nguvu kubwa ya mwanamke.”