Baba akisalia Ukraine kupigana vita, mtoto ukimbizi na matumaini ya kumwona tena

Tarehe 5 Machi 2022 watoto na familia zao wakiwa wamefika Berdyszcze, Poland baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine kukimbia vita.
© UNICEF/Tom Remp
Tarehe 5 Machi 2022 watoto na familia zao wakiwa wamefika Berdyszcze, Poland baada ya kuvuka mpaka kutoka Ukraine kukimbia vita.

Baba akisalia Ukraine kupigana vita, mtoto ukimbizi na matumaini ya kumwona tena

Wahamiaji na Wakimbizi

Ni wiki mbili sasa tangu Urusi ianzishe mashambulizi yake nchini Ukraine, kitendo hicho kimesambaratisha familia ikiwemo wanaume kulazimika kusalia Ukraine ili kupigana vitani huku familia zao zikilazimika kukimbia maeneo mengine ya taifa hilo au hata nje ya Ukraine. 
 

Hali hiyo imeleta upweke kwa familia hususan ambazo wanaume wanapaswa kusalia Ukraine ili kushiriki katika mapigano ya kukomboa nchi yao.

Miongoni mwa familia zilizoathirika ni ile ya Yevgenii na mkewe Oleksandra ambao kwa pamoja wana watoto wawili wa kike Milana na Polina.

Mashambulizi kutoka Urusi yalipoanza tarehe 24 mwezi Februari walilazimika kuondoka kwenye makazi yao jimboni Donetsk na kukimbilia jimbo la Zakarppatia lililoko Magharibi mwa Ukraine.

Chuo Kikuu cha Mukachevo kinawahifadhi

Walipata hifadhi katika Chuo Kikuu cha Mukachevo ambapo walipatiwa chumba wanamoishi Oleksandra, Milana, Polina na mama mzazi wa Oleksandra. “Mume wangu alirudi nyumbani baada ya kutufikisha hapa salama. Serikali inataka wanaume wenye umri wa kati ya miaka 18 hadi 60 wabakie Ukraine waingie jeshini kupambana kukomboa nchi,” amesema Oleksandra.

Akiwa kwenye chumba chao, Milana mwenye umri wa miaka 6, amechora picha kwa kutumia rangi na amemchora baba yake mzazi. Anakumbuka pia kuwa wakati wa msafara wao kwenye magari mawili, walichukua pia mbwa wao.

Sisi tuko salama baba je?

Familia hii hapa hofu ni kwa Yevgenii ambaye amerejea nyumbani kupigania taifa lao.
Lakini Milana ana matumaini kuwa iko siku atamuona baba yake akisema, “nitakaporejea, nitaenda kumtembelea bibi yangu. Nina bibi wawili na pia niña babu na baba yangu Yevgenii.”

UNHCR inaendelea kuimarisha misaada Ukraine

Pamoja na mashambulizi yanayoendelea Ukraine kutoka Urusi, Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia wakimbizi, UNHCR linashirikiana na mamlaka za mji huu kupanua huduma za kupokea wakimbizi, sambamba na kubainisha majengo ya kukarabatiwa ili yatumike kama malazi kwa wakimbizi wa ndani.

Kwa kushirikiana pia na shirika la kiraia la NEEKA, UNHCR inapatia kituo hiki nguo za joto, maji, chakula, na vifaa vinavyohitajika zaidi vya jikoni kama vile majokofu na majiko ya kupashia vyakula.