Mradi wa FISH4ACP walenga kuwainua wanawake wachakataji mkoani Kigoma, Tanzania
Mradi wa FISH4ACP walenga kuwainua wanawake wachakataji mkoani Kigoma, Tanzania
Katika baadhi ya jamii wanawake hutafsiriwa kama kundi dhaifu lisilo na mchango wowote katika maendeleo wakiamini anapaswa kufanya majukumu ya nyumbani pekee lakini ni ukweli usiopingika kuwa kundi hili lina mchango mkubwa katika kuinua uchumi wa familia na Taifa kupitia sekta mbalimbali.
Katika mkoa wa Kigoma, baadhi ya wanawake wamejikita kufanya kazi katika sekta ya uvuvi. Ziada Juma ni mchakataji katika Mwalo wa Katonga na anaeleza sababu za kufanya kazi hii.
“Kilichonisukuma haswa haswa ni maisha yalivyonibana ndiyo maana niliona katika kuhangaika huku na huku nikaingia kwenye hizi biashara za kuchakata hapa ziwani na kulingana na maisha magumu ndiyo maana niliingia kwenye hizo biashara,”Amesema Ziada.
Changamoto wanazokutana nazo ni zipi?
“ Hizi biashara zenyewe hazipatikani zinanunuliwa kwa shida, hakuna masoko ya kuuzia tunakaa barabarani hizo mara nyingi na mitaji kuwa midogo ndo changamoto tunazokutana nazo,”Ameeleza.
Nimefanikiwa pia kuzungumza na Fatuma Ndasalama ambaye ni mfanyabiashara nikamuuliza kuna umuhimu gani kwa mwanamke kufanya kazi?
“Maanake unapokuwa unajishughulisha kwa mafano kama sisi tuna watoto, mtoto anapokuwa amesoma amefaulu baba yake anaweza kujikuta hana kitu baadaye wewe ukampiga nguvu mwanaume mimi nawashauri tu wanaowakataza wake zao wawape tu ruhusa waendelee kufanya biashara mwanaume anapokuwa amekwama mwanamke anamkwamua,”amefafanua Fatuma.
Aboubakari Milembe naye ni mkazi wa Katonga anatuambia wanawake wana mchango gani katika maendeleo na ujumbe wake kwa kina baba.
“Mwanaume anapoenda kutafuta riziki kuna wakati anakwama mwanamke katika kuhangaika kwake anafanikiwa kwahiyo inasaidia kifamilia kwa sababu kuna watu wenye familia kubwa, wenye familia za kawaida na familia za chini kwa hiyo naona hilo suala ni muhimu sana katika kutafuta riziki baina ya watu wawili mwanaume na mwanamke mimi nawasihi wawape ruhusa wenzao waende kutafuta riziki,”Amebainisha Aboubakari.
Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa FISH4ACP kupitia FAO, Hashim Muumin anahitimisha kwa kutuambia namna shirika hilo linagusa wanawake kiuchumi.
“Katika mkakati huu umezingatia masuala ya jinsia hasa hasa kina mama katika uvuvi huu wa Ziwa Tanganyika kwa asilimia zaidi ya 90 ndiyo ambao ni wachakataji wakubwa ushiriki wao katika maamuzi, usimamizi katika mnyororo huu wa thamani wa uvuvi wa Ziwa Tanganyika umeonekana mdogo sana kwahiyo mradi huu umelingalia suala hilo na utaenda kulishughulikia kuhakikisha kwamba katika eneo hilo kunaimarika,”Ameeleza Hashim.
Maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani mwaka 2022 yanafanyika chini ya kauli mbiu isemayo "Kizazi cha Haki na Usawa kwa Maendeleo Endelevu"