Watoto 11 watolewa jeshini Maridi Sudan Kusini kwa msaada wa UNMISS 

10 Machi 2022

Watoto 11 wameachiliwa kutoka jeshini kwenye makundi mbalimbali yenye silaha katika mji wa Maridi jimboni Equatoria Magharibi nchini Sudan Kuisni kwa msaada mkubwa wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS. 

Watoto hao wakiwa wamevalia sare ya fulana na kofia nyekundu walizopewa na UNMISS wamepokelewa eneo la Maridi baada ya kuachiliwa huru na makundi ya wapiganaji na kukabidhiwa kwa jeshi la Sudan na UNMISS tayari kwenda kuanza maisha mapya uraiani. 

Meja jenerali Duach Garang ni kamanda wa kikosi cha jeshi la ulinzi na usalama la Sudan Kusini anasema “tumedhamiria kuwaachilia watoto wote ambao wako jeshini, hatuna shida na suala hilo, tunakubaliana na yote yaliyosemwa na mpango wa UNMISS, Sudan Kusini. Hivyo tunakubaliana na suala la haki za mtoto” 

Maelfu ya wavulana na wasichana bado wanajihusisha na vikosi vya kijeshi au makundi yenye silaha nchini humu, wengine  kwa shinikizo na wengine kwa hiyari yao. 

UNMISS inasema sasa mchakato unaanza kuwaandikisha kwa ajili ya kuwajumuisha watoto hawa walioachiwa mapema wiki hii katika maisha ya kawaida kwenye jamii ambako watasaidiwa kurejea shuleni na kujifunza mbinu za kuweza kujiingizia kipato ili kujikimu kimaisha.
 
Mkurugenzi wa kundi la watu wenye mahitaji maalum katika mchakato wa upokonyaji silaha na ujumuishwaji kwenye jamii wapiganaji wa zamani Nelson Modi Joseph anasema “Watoto wetu ambao ni wadogo bado wana fursa ya mustakbali bora nasi tumejizatiti kuhakikisha wanapata haki yao ya elimu, afya na haki zote kama raia wa Sudan Kusini.” 

Akiunga mkono hilo afisa programu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF nchini humo Clement Mbiko amesema hofu yao kubwa ni mustakbali wa watoto akisisitiza kuwa  ni wajibu wao kuhudumia watoto ambao wameshiriki katika vikosi au makundi yenye silaha na sasa wanatambua kuwa watakuwa na mustakabali bora, na wanahitaji kukua na kuwa watu wazima wanaowajibika.

Naye mkuu wa kitengo cha UNMISS cha ulinzi kwa watoto amesema hatua hii iliyochukuliwa na pande husika kuwalinda watoto, sasa Sudan Kusini imepiga hatua ya kutoka kundi A kwenda B la nchi ambazo zilizokuchua hatua za kuboresha na kuwalinda watoto.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter