Watu wananishangaa kuona mwanamke ninaendesha gari - Babli Akter

Picha ya maktaba: Romela Islam alimtoroka ndoa yake ya kikatili baada ya kaka yake kumchukua na kumhamishia kituo cha kuhifadhi manusura wa ukatili Bangladesh
UN Women/Fahad Kaizer
Picha ya maktaba: Romela Islam alimtoroka ndoa yake ya kikatili baada ya kaka yake kumchukua na kumhamishia kituo cha kuhifadhi manusura wa ukatili Bangladesh

Watu wananishangaa kuona mwanamke ninaendesha gari - Babli Akter

Wanawake

Nchini Bangladesh katika eneo la kaskazini mwa nchi katika mji wa Mollikpur, mradi uliofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD kwa kushirikiana na serikali ya nchi hiyo, umeanza kuzaa matunda kwa wanawake wa umri mdogo ambao wamepata mafunzo ya udereva.

 

Katikati ya pilikapilika za mji wa Mollikbur Bangladesh, Babli Akter, mwanamke kijana akiwa amevalia ushungi wake maridadi anatembea kuelekea kwenye gari dogo lililoegeshwa pembeni ya barabara. Si kwamba yeye ni abiria, la hasha, yeye hasa ndiye dereva wa gari hili la biashara ya kusafirisha watu.  

Hili ni jambo linalowashangaza wakazi wa eneo hili sio kwa sababu ya muonekano wake au hilo gari anamoingia bali kinachowashangaza watu ni kuona mwanamke akiingia kukalia kiti cha dereva. Ni jambo nadra sana akama anavyoeleza mwenyewe akisema…"ndio, watu wananikodolea macho. Wakati mwanamke anaendesha gari barabarani, watu hutazama kwa kutoamini, inawezekanaje kuwa mwanamke anaendesha gari?" 

Kundi la wanawake vijana Kaskazini mwa Bangladesh sasa wanaingia katika taaluma inayotawaliwa na wanaume, baada ya kupokea masomo ya udereva kwa mara ya kwanza. 

Babli ni mmoja wa wanawake vijana 40 wasio na ajira ambao ni wa kwanza kupokea masomo ya kuendesha gari kutoka kwa mradi huu unaofadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD na Serikali ya Bangladesh. Ndaya Beltichika ni Mtaalamu wa Jinsia katika IFAD anafafanua akisema, “kwa hiyo mradi huu ni mradi unaowawezesha wanakijiji kujipatia kipato, kupanua vyanzo vyao vya mapato katika mazingira ya mabadiliko ya tabianchi, kwa sababu eneo hilo linaathirika sana na ukame na mafuriko makubwa. Kwa hiyo kwa ujuzi huu watakuwa na fursa ya kujipatia kipato, kuhudumia familia na kisha kulindwa dhidi ya uhitaji wa kuolewa mapema kwa sababu ya ukosefu wa fursa.” 

Mradi huu unatarajia kutoa mafunzo kwa wanawake zaidi katika miaka michache ijayo. Pamoja na kutoa ajira, mradi huu unaweza kuleta usawa zaidi katika siku zijazo kwa wanawake katika taaluma nyingine zinazotawaliwa na wanaume.