Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila vikwazo kuanzia ngazi ya familia, wanawake wana mchango mkubwa na chanya kwa jamii

Wanakikundi cha Kujitegemea  kilichopo kijiji cha Kumuhama
John Kabambala
Wanakikundi cha Kujitegemea kilichopo kijiji cha Kumuhama

Bila vikwazo kuanzia ngazi ya familia, wanawake wana mchango mkubwa na chanya kwa jamii

Wanawake

Miradi mbalimbali inayotekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa na wadau wake kote duniani, imeweka wazi ukweli kwamba vikwazo mbalimbali vinavyowakabili wanawake vinapoondolewa, wanawake wanakuwa chachu ya kuleta mabadiliko chanya katika karibia kila sekta katika jamii.  

Mfano wa karibu ni katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania ambako kupitia mradi wa pamoja Kigoma, KJP chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Shirika la Umoja wa mataifa la maendeleo ya mitaji UNCDF na Kituo cha Biashara cha kimataifa ITC, wanawake sasa wanatoa mchango mkubwa wa maendeleo katika jamii yao.  

Mradi huo wa ushirikiano wa pamoja Kigoma moja ya kundi lililohusishwa ni wanawake vijana kupitia vikundi vilivyoundwa kwenye maeneo ya utekelezaji wa mradi katika Wilaya nne mkoani humo, Kasulu TC,Kasulu DC,Kibondo DC na Kakonko DC. 

Leokadia Isdory  mkazi wa kijiji cha Katanga Wilaya ya Kakonko Mkoa wa Kigoma anaeleza mabadiliko aliyoyapata baada ya kupata elimu katika mradi huu akisema, “baada ya kupeleka mrejesho wa semina nyumbani, kwakweli mume wangu kwanza alisita. Lakini mpaka sasa hivi mzee amehamasika vizuri kwa sababu mwanzoni alikuwa anafanya kama hataki. Lakini sasa hivi baada ya kuona kwamba matunda ni mazuri, mahindi ni mazuri, amehamasika. Sasa hivi tukienda kuangalia lile shamba, na yeye anahamasika kwenda kuangalia mara kwa mara. Hata watoto wanasema mwaka huu ugali ni wa kutosha.” 

Rozalia Kiliani ni mkulima wa maharagwe mkazi wa kijiji cha Kumuhama “B” Wilaya ya Kibondo Mkoa wa Kigoma yeye pia ni mnufaika wa mradi wa KJP, ni yapi aliopitia hadi kuona mafanikio. 

“Huu mwaka tumelima mahindi na maharage. Na sasa maharage tumeanza kuvuna na mavuno ya maharage yamepatikana kwa wingi. Japo mahindi hatujavuna, tunatarajia kupata mazao mengi ukilinganisha na miaka ya nyuma nilikuwa ninapata magunia kidogo lakini kwa sasa ninavyoona nitapata magunia kuanzia ishirini. Na haya ni mafanikio yaliyopatikana baada ya kujiunga kwenye kikundi. Hapo mwanzo nilipigwa sana na mume wangu akitaka nisijiunge na hicho kikundi lakini nilivumilia nikawa ninaenda kiuficho na sasa matokeo yanaonekana maana ninachokipata ninamwonesha mume wangu. Kwani kila nikimwonesha anafurahia. Na yeye sasa hivi ameamua kujiunga na sisi baada ya kuandika barua ya maombi ya kujiunga na kikundi. N akwenye familia yetu sasa hatuna njaa. Lakini pia tunaendelea kupata ujuzi wa aina mbalimbali mimi na mume wangu ambao unatusaidia kuendesha familia yetu.” Anaeleza Rozalia huku akitabasamu.  

Kwa upande wake Helen Bulaheze mkazi wa kijiji cha Kibingo Halimashauri ya Wilaya ya Kibondo, ameona mabadiliko ya afya za watoto wake walio kuwa na uzito pungufu baada ya kulima viazi lishe nakutumia nyumbani kama chakula chenye virutubishi sasa watoto wake wameongezeka uzito kama anavyofafanua akisema, “hii mbegu niliyoishika ni aina ya kabode. Mavuno yake ni mazuri sana. Ndani kiazi kina rangi ya karoti na kinaongeza nguvu mwilini. Nyumbani ninakitumia kwa ajili ya lishe. Nina watoto wadogo chini ya miaka mitano kinazuia utapiamlo kwa watoto wadogo. Awali watoto nilikuwa nikiwapeleka kiliniki uzito ulikuwa unapungua laikini tangu nimeanza kutumia viazi hivi nikiwapeleka kiliniki maendeleo yao ni mazuri sana.” 

TAGS: FAO, UNCDF, ITC, WFP, KJP, FAO Tanzania