Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kamisheni huru yaundwa kuchunguza ukiukwaji wa haki utokanao na uvamizi wa Urusi Ukraine

Yuril ambaye ni mume wa Bi. Shostak akiwa amembeba mtoto wao mchanga hospitalini. Mpango wao ni kuendelea kuishi kwenye handaki nyumbani mwao.
© Mariia Shostak via UNFPA
Yuril ambaye ni mume wa Bi. Shostak akiwa amembeba mtoto wao mchanga hospitalini. Mpango wao ni kuendelea kuishi kwenye handaki nyumbani mwao.

Kamisheni huru yaundwa kuchunguza ukiukwaji wa haki utokanao na uvamizi wa Urusi Ukraine

Haki za binadamu

Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu, HRC leo limepitisha azimio linaloamua kuanzishwa kwa Kamisheni Huru ya Kimataifa ya kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu katika tukio la sasa la uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Upigaji kura umefanyika katika mkutano huo wa 49 wa Baraza hilo la haki za binadamu ambapo nchi 32 ziliunga mkono, nchi 2 zilipinga ilhali 13 hazikupiga kabisa kura.

Azimio hilo pamoja na kuridhia kuanzishwa kwa Kamisheni hiyo pia linalaani vikali ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na ukiukaji wa sheria za haki za binadamu za kimataifa utokanao na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine na kuikata Urusi kuacha mara moja ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kibinadamu nchini Ukraine.

Baraza pia kupitia azimio hilo limetaka kuondolewa haraka kwa majeshi ya Urusi nchini Ukraine, kuondolewa ambako kunaweza kuthibitishwa sambamba na kuondoka kwa waasi wanaoungwa mkono na Urusi kwenye eneo lote la Ukraine linalotambulika kimataifa.

Sambamba na hilo limetaka kuwepo kwa njia isiyo na vikwazo vyovyote ya kupeleka misaada ya kibinadamu.

Tweet URL

Muundo wa Kamisheni

Kamisheni hiyo huru ya kimataifa itaundwa na wataalamu watatu wa haki za binadamu watakaoteuliwa na Rais wa Baraza la Haki za Binadamu na watafanya kazi kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Majukumu yao pamoja na mambo mengine ni kuchungua madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu na uhalifu unaohusiana nao katia muktadha wa Urusi kuvamia Ukraine.

Katika kufanya hivyo watabaini misingi, mazingira na mizizi ya chanzo cha ukiukwaji huo na kutoa mapendekezo hususan mikakati ya uwajibishaji wale wote kwa misingi ya kuondokana na ukwepaji mkono wa sheria.

Waliowasilisha azimio

Azimio liliwasilishwa na Ukraine ambapo Belarusi ilizungumza kama nchi inayoguwa katika mzozo huo ambapo taifa hili limekuwa likiunga mkono msimamo wa Urusi katika janga hilo.
 
Katika mjadala uliotangulia kupitishwa kwa azimio hilo, wazungumzaji walionesha mshikamano na wananchi wa Ukraine na kuelezea hofu yao kuhusu hali inayoendelea sasa nchini humo.
Pamoja na kutoa wito wa kuundwa kwa kamisheni hiyo, baadhi ya wajumbe walitaka kuwepo na mtaalamu maalum wa hali ya kibinadamu nchini Urusi.

Nchi zilizopiga kura ya hapana ni Urusi na Eritrea huku zile ambazo hazikupiga kura kabisa ni pamoja na Cuba, Sudan, Namibia, China na Venezuela.

Mapema Baraza lilitulia kwa dakika moja kukumbuka waathirika wa uvamizi huo wa Urusi nchini Ukraine.