Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wote wanaokimbia Ukraine wana haki ya kupokelewa bila ubaguzi- Bachelet

Watu waliokimbia Ukraine wakijipasha joto kweny emoto baada ya kuvuka mpaka na kuingia Poland kwenye eneo la mpaka la Medyka
© UNHCR/Valerio Muscella
Watu waliokimbia Ukraine wakijipasha joto kweny emoto baada ya kuvuka mpaka na kuingia Poland kwenye eneo la mpaka la Medyka

Watu wote wanaokimbia Ukraine wana haki ya kupokelewa bila ubaguzi- Bachelet

Amani na Usalama

Hii leo huko Geneva, Uswisi, mkutano wa 49 wa Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu limekuwa na kikao cha dharura kuhusu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ambapo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema makaribisho wanayopata raia wa Ukraine ugenini yaelekezwe pia kwa raia kutoka nchi zingine ambao wanakimbia machafuko nchini Ukraine.

Baraza hilo limekuwa na kikao cha dharura siku moja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa na kikao cha dharura kilichopitisha azimio la kuitaka Urusi pamoja na mambo mengine iondoke Ukraine bila masharti yoyote.

Akihutubia Baraza hilo la Haki za Binadamu Bi. Bachelet amesema makaribisho ambayo wanapatiwa raia wa Ukraine ugenini yaelekezwe kwa wale wote wanaokimbia mzozo bila kujali uraia wao, kabila, hadhi ya uhamiaji au kitu chochote kile.

“Kumekuweko na dalili za kuchukiza za ubaguzi dhidi ya watu kutoka barani Afrika na Asia ambao wanakimbia Ukraine, na ofisi yangu itafuatilia kwa kina suala hili,” amesema Bi. Bachelet.

Hofu ya Bachelet juu ya wale waliosalia Ukraine

Makumi ya mamilioni ya watu wamesalia Ukraine na wako hatarini kukumbwa na mashambulizi ambapo Bi. Bachelet amesema hofu yake kubwa ni kwamba mashambulizi yanayoendelea hivi sasa yataongeza hatari inayowakumba.

Tarehe 27 mwezi Februari mwaka 2022, operesheni za kijeshi za Urusi zikiendelea Ukraine, familia zikiwa na watoto wadodo zinasubiri kupanda treni kwenye kitou cha Lviv karibu na mpaka na Poland
© UNICEF/Viktor Moskaliuk
Tarehe 27 mwezi Februari mwaka 2022, operesheni za kijeshi za Urusi zikiendelea Ukraine, familia zikiwa na watoto wadodo zinasubiri kupanda treni kwenye kitou cha Lviv karibu na mpaka na Poland

“Watu wengi wakiwemo wazee, wajawazito, wanawake, watoto na watu wenye  ulemavu wanalazimishwa kujikusanya kwenye vituo vya hifadhi vilivyoko kwenye mahandaki, vituo vya treni vilivyo chini ya ardhi kwa lengo la kukwepa milipuko. Wengine wanatenganishwa na familia zao. Wafanyakazi wangu wamekuwa wakipata mawasiliano kutoka kwa raia wenye hofu ya mateso iwapo majeshi ya Urusi yatasonga mbele, mathalani wanajamii wa Tatar huko Crimea,watetezi wa haki za binadamu na wanahabari,” amesema Bi .Bachelet.

Kinachopaswa kufanyika sasa

Kwa kutambua madhila yanayoendelea hivi sasa dhidi ya raia ikiwemo mauaji na majeruhi sambamba na miundombinu ya kiraia kama vile shule na hospitali, Bi. Bachelet amesema “tuko hapa kuonesha na kuzingatia ahadi yetu ya ushirikiano wa kimataifa na haki za binadamu. Napazia sauti wito uliotolewa jana na Baraza  Kuu la Umoja wa Mataifa wa suluhu ya haraka ya mzozo unaoendelea kwa njia ya amani.”

Nchi laizma zizingatie utawala wa kisheria na misingi ya kulinda uhai wa binadamu na utu na kwa msingi huo Kamishna huyo amesema ni vema operesheni za usambazaji wa misaada ya kibinadamu zikafanyika bila vikwazo vyovyote ili kufikia raia wanaohitaji nchini kote Ukraine.
 
Amekumbusha kuwa ulinzi wa raia sambamba na ulinzi wa askari wanaokamatwa ni jambo linalotakiwa kuzingatiwa kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za Umoja wa Mataifa.

 

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akiwa na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 3 wakiwasili katika kituo cha muda cha makazi nchini Romania baada ya kukimbia vita Ukraine
© UNICEF/Ioana Moldovan
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 9 akiwa na mdogo wake wa kiume mwenye umri wa miaka 3 wakiwasili katika kituo cha muda cha makazi nchini Romania baada ya kukimbia vita Ukraine

Kuunga mkono harakati za vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa

Wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio, huku Baraza la Haki za Binadamu likiwa na kikao cha dharura, vyombo vingine vya Umoja wa Mataifa vimetangaza hatua zao dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine ulioanza tarehe 24 mwezi uliopita wa Februari.

“Natambua kuwa katika ngazi ya kimataifa, Mahakama ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki, ICJ, imetangaza rasmi kuanza siku ya Jumatatu mchakato unaohusiana na mzozo unaoendelea Ukraine. Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, ICC imetangaza uamuzi wake wa kuanza kuchunguza hali ya Ukraine kufuatia maombi kutoka kwa nchi wanachama,” amesema Bi. Bachelet.

Na kwa upande Baraza la Haki za Binadamu, Bi. Bachelet amesema Baraza lina pendekezo muhimu la kuendeleza misingi, kupanua wigo wa uwajibikaji kupitia kamisheni huru ya kimataifa ya uchunguzi.

Bi. Bachelet amesema pamoja na hayo, wafuatiliaji wa haki za binadamu wa ofisi ya Haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, wataendelea kuwepo Ukraine na kwamba “janga la sasa linaonesha umuhimu wa lengo letu la kufuatilia na kutoa ripoti kuhusu Ukraine na katika nchi zingine. Nachukua fursa hii kushukuru wafanyakazi wote wa OHCHR hasa wale walioko mashinani kwa kujitolea kwao.”

Kwa kipindi cha miaka nane, OHCHR imekuwa ikifuatili hali ya haki za binadamu nchini Ukraine hasa kwenye maeneo ya Donbas na Crimea na mj iwa Sevastopol ambao umekuwa unakaliwa na Urusi tangu mwaka 2014.