Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wanauawa, wanajeruhiwa na wengine wanapata kiwewe kutokana na machafuko Ukraine: UNFPA

Mtoto wa miaka 7 akiwa amekaa kwenye kitanda katika nyumba ya wasaka hifadhi huko Lviv, Magharibi mwa Ukraine
© UNICEF/Kostiantyn Golinchenko
Mtoto wa miaka 7 akiwa amekaa kwenye kitanda katika nyumba ya wasaka hifadhi huko Lviv, Magharibi mwa Ukraine

Watoto wanauawa, wanajeruhiwa na wengine wanapata kiwewe kutokana na machafuko Ukraine: UNFPA

Msaada wa Kibinadamu

S​​​hirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA limesema kuongezeka kwa mgogoro nchini Ukraine kunaleta tishio la haraka na linaloongezeka kwa maisha na ustawi wa watoto milioni 7.5 wa nchi hiyo.

Mbali na kuongezeka kwa mahitaji ya kibinadamu UNFPA ilibainisha kuwa watoto wameuawa, kujeruhiwa, na wanatiwa kiwewe sana na ghasia zinazowazunguka. Mamia kwa maelfu ya watoto wametenganishwa na familia zao na kukimbilia nchi jirani kusaka hifadhi.

Familia ikivuka kivuko cha mpaka cha Zosin huko Poland baada ya kukimbia Ukraine.
© UNHCR/Chris Melzer
Familia ikivuka kivuko cha mpaka cha Zosin huko Poland baada ya kukimbia Ukraine.

Wakina mama wasaka hifadhi

Msururu mrefu wa magari yanayosubiri kuingia mpakani mwa nchi ya Moldova yakitokea Ukraine kukimbia machafuko, wakina mama wengine wakiwa na Watoto wao wanatembea kwa miguu kuingia katika mpaka huo ili kusaka hifadhi.

Maria ni mama aliyemuacha mume wake huko Odessa, Ukraine. Ameingia akiwa na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miezi 18 mikononi mwake. Anasema ameiacha familia yake -  wazazi, bibi na kaka zake wawili amekuja Moldova kuokoa maisha ya mtoto wake.

“Nilikuwa nimelala. Kila kitu kilikuwa sawa. Niliamka takriban saa 11 alfajiri nilishtushwa na kishindo. Hata jengo letu lilikuwa linatetemeka. Ninaishi katika kitongoji cha "Malinovskii", ambapo sio mbali kulikuwa na milipuko ya mabomu. kimya Siku iliyofuata kulikuwa na ukimya. Lakini ninaogopa mtoto. Sijui itakuwaje baada ya hapo, nahofia haitawezekana kabisa kuondoka nchini.”

Mnamo tarehe 27 Februari 2022, halijoto ikiwa karibu na nyuzi joto sifuri Selcius, mtoto aliyevikwa blanketi anajiweka joto wakati yeye na familia yake wakisubiri kupanda treni ya uokoaji huko Lviv, kona ya magharibi kabisa ya Ukraine
© UNICEF/Viktor Moskaliuk
Mnamo tarehe 27 Februari 2022, halijoto ikiwa karibu na nyuzi joto sifuri Selcius, mtoto aliyevikwa blanketi anajiweka joto wakati yeye na familia yake wakisubiri kupanda treni ya uokoaji huko Lviv, kona ya magharibi kabisa ya Ukraine

Juhudi zinafanyika 

Kila uchwao idadi ya wakimbizi kutokea Ukraine inaendelea kuongezeka wakikimbilia katika nchi jirani za Poland, Hungary, Moldova, Romania, Slovakia, na nchi nyingine za Ulaya.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi UNFPA, Ukraine ina wastani wa wajawazito 265,000, kati yao wapatao 80,000 wanatarajiwa kujifungua katika kipindi cha miezi mitatu ijayo na hivyo kuna uhitaji wa haraka wa kuongeza juhusi za kuokoa maisha ili kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wote wanalindwa dhidi ya ukatili, na watoto wanazaliwa salama na kwa uangalifu wa hali ya juu.

Shirika hilo linasambaza vifaa muhimu kwa wanawake ikiwemo taulo za kike.