Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa unyanyasaji wa wanawake na wasichana nchini Ukraine: Pramila Patten

Mtoto mkimbizi kutoka Ukraine amesimama na mbwa wake kwenye kituo cha wakimbizi cha muda karibu na kivuko cha Palanca kwenye mpaka wa Jamhuri ya Moldova na Ukraine, tarehe 26 Februari 2022.
© UNICEF/Constantin Velixar
Mtoto mkimbizi kutoka Ukraine amesimama na mbwa wake kwenye kituo cha wakimbizi cha muda karibu na kivuko cha Palanca kwenye mpaka wa Jamhuri ya Moldova na Ukraine, tarehe 26 Februari 2022.

Nina wasiwasi kuhusu kuongezeka kwa unyanyasaji wa wanawake na wasichana nchini Ukraine: Pramila Patten

Wanawake

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu Unyanyasaji wa Kijinsia katika Migogoro, Pramila Patten, ana wasiwasi mkubwa kuhusu hali inayozidi kuzorota nchini Ukraine na ametoa wito wa haraka wa ulinzi wa raia, hasa wanawake na wasichana, ambao wameathiriwa kwa kiasi kikubwa na migogoro ya kivita na kukimbia.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Patten amesema “Mgogoro huu tayari unaathiri pakubwa ulinzi na usalama wa raia, hasa wanawake na wasichana, ambao wako katika hatari kubwa ya unyanyasaji”.

Mwakilishi Maalum Patten ametoa wito kwa pande zote kuzingatia haki za binadamu na utu wa watu wote, kujizuia, na kuhakikisha wanafuata sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na upigaji marufuku wa aina zote za unyanyasaji wa kijinsia.

Mapigano hayo yamesababisha watu wengi kulazimika kuyahama makazi yao, hali iliyowalazimu raia wengi kukimbilia nchi jirani. Amesema iwapo mzozo huo hautakoma, maelfu ya familia za ziada zitahamishwa kwa nguvu, na hivyo kuongeza kwa kasi kiwango cha hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari ipo na kuongeza hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji.

“Ninaunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kukomesha mara moja uhasama na kutoa wito kwa upatikanaji usiozuiliwa wa misaada ya kibinadamu kwa wale wanaohitaji, hasa wanawake na wasichana. Pia nitoe wito kwa wahusika wote kujiepusha na kushambulia huduma muhimu za afya na miundombinu mingine ya kiraia, ambayo ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma, ikiwa ni pamoja na huduma ya afya ya ngono na uzazi na usaidizi wa kisaikolojia kwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia”.

Mwakilishi Maalum Patten pia ametoa wito wa kupewa kipaumbele kwa msaada wa kuokoa maisha kwa waathirika wa unyanyasaji wa kingono na kijinsia wakati wa kutoa misaada ya kibinadamu.