Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwajali wavuvi wadogo wadogo – FAO

Wavuvi wa Senegal wanashusha samaki kutoka kwenye boti zao na kuwauza katika masoko ya ndani na kusafirisha hadi nchi nyingine.
© FAO/John Wessels
Wavuvi wa Senegal wanashusha samaki kutoka kwenye boti zao na kuwauza katika masoko ya ndani na kusafirisha hadi nchi nyingine.

Tuwajali wavuvi wadogo wadogo – FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa siku nne wa wakuu wa nchi zenye bahari duniani, unaanza leo huko Roma Italia na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limetoa wito kwa wasomi, serikali, mashirika ya kiraia na sekta binafsi kutambua umuhimu wa wavuvi wadogo wadogo na ufugaji wa samaki, ambao ni sehemu muhimu ya uvuvi.

Bahari, inachukua jumla ya  asilimia 70 ya uso wa dunia na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu ulimwenguni kote.

Lakini bahari inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uvuvi wa kupita kiasi, uchafuzi wa bahari na mabadiliko ya tabianchi na hivyo vyote vinatishia uwezo wa bahari kuendelea kutoa huduma muhimu za mfumo wa ikolojia na rasilimali muhimu za chakula.

Wavuvi wadogo wadogo na ufugaji wa samaki ni sehemu muhimu ya mifumo ya chakula duniani na inaweza kuchukua jukumu muhimu katika kulinda bahari, hata hivyo, hawatambuliwi au kueleweka vyema kama anavyoeleza mvuvi José Tejeda Dumé kutoka Santo Domino, DOMINICAN REPUBLIC.

“Sekta fulani zinatupuuza. Hawaoni kwamba mvuvi huamka saa 10 alfajiri na kukumbana na dhoruba na mvua. Ni lazima aende baharini ili kuwapatia rizki watoto wake.”

Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador
FAO/Camilo Pareja
Samaki ambao ndio kwanza wametoka kuvuliwa katika eneo la santa Rosa de Salinas, Ecuador

FAO kupitia mradi wake wa FISH4ACP imejitolea kuimarisha shughuli za uvuvi wa kisanaa, kuhakikisha kuwa watu wanaohusika katika sekta hii wanapata usaidizi na kutambuliwa ipasavyo kama anavyoeleza  Vera Agostini, Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Uvuvi na Ufugaji wa samaki cha FAO

"Uvuvi mdogo mdogo na ufugaji wa samaki hautambuliki kuwa ni muhimu sana. Tukiangalia tu baadhi ya takwimu zinaweza kukusaidia kuelewa, zinaweza kutusaidia sote kuelewa kwamba asilimia 90 ya wanaojihusisha na uvuvi ni wale ambao ni wavuvi wadogo, watu milioni 60 na asilimia 40 ya hao ni wanawake. Kwa hivyo, kwa kweli ni sehemu muhimu ya uvuvi, lakini hazitambuliki na hazithaminiwi. Tunahitaji kupata neno kuhusu umuhimu wao, na tunahitaji kuwasaidia watoa maamuzi kutambua hilo na kuchukua hatua”.

Agostini ameongeza kuwa FAO inaamini mifumo ya chakula cha majini ni sehemu muhimu ya mifumo ya chakula duniani. Kwa nini?

“Kwa sababu wao huboresha lishe, haswa kwa walio hatarini zaidi, ni sehemu muhimu ya ukuaji wa uchumi, na hutoa suluhisho ambazo hupunguza kiwango cha uharibifu wa mazingira cha mifumo ya chakula. Kwa hivyo, mkutano huu wa kilele ni fursa muhimu sana kuleta ajenda hiyo ya mabadiliko ya bluu na kushiriki katika mazungumzo na kundi tofauti la wadau watakaokuwepo”.

FAO imejidhatiti kuimarisha shughuli za uvuvi wa kisanaa, kuhakikisha kuwa watu wanaohusika katika sekta hii wanapata usaidizi na kutambuliwa ipasavyo.