Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kimbunga Emnati kuongeza zahma Madagascar:WFP

Nchini Madagaska, Rachelle Elien, afisa wa masuala ya kibinadamu wa OCHA na mwanachama wa timu ya dharura ya UNDAC, hukutana na watu walioathirika baada ya Kimbunga cha Emnati.
Chris Monnon / Atlas Logistique / OCHA
Nchini Madagaska, Rachelle Elien, afisa wa masuala ya kibinadamu wa OCHA na mwanachama wa timu ya dharura ya UNDAC, hukutana na watu walioathirika baada ya Kimbunga cha Emnati.

Kimbunga Emnati kuongeza zahma Madagascar:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula WFP limesema kimbunga Emnati kilichoikumba Madagascar Jumatano ya wiki hii (23/02/2022) kikiwa kimbunga cha nne kulikumba taifa hilo katika wiki kadhaa kinatishia uhakika wa chakula na ni mfano wa kjinsi gani cangamoto za mabadiliko ya tabianchi zisiposhughulikiwa zinaweza kusababisha mahitaji makubwa ya kibinadamu. 

Kimbunga hicho kinatarajiwa kuzidisha tatizo la njaa na hatari ya mafuriko na tathimini hii imetolewa siku chache kabla ya kutoleewa kwa ripoti ya jopo la kimataifa  kuhusu mabadiliko ya tabianchi IPCC

Athari za vimbunga Madagascar 

WFP inasema kikizikumba jamii zilizo hatarini ambazo tayari zimefikia mwisho, Kimbunga Emnati kinatarajiwa kuzidisha njaa ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya kusini mwa Madascar, ambayo yamekuwa yakikabiliwa na ukame mkali wa miaka mingi ikiwa ni dhihirisho jingine la hatari ya nchi hiyo kutokana na mabadiliko ya tabianchi 

“Vimbunga Emnati, Dumako, Batsirai na Ana vimeharibu taifa la kisiwa cha Madagascar na kusababisha uharibifu mkubwa wa ardhi ya kilimo ikiwa ni pamoja na zao la mpunga ambalo lilikuwa limebakiza wiki chache kabla ya kuvunwa. Mazao ya biashara kama vile karafuu, kahawa na pilipili pia yameathirika kwa kiasi kikubwa. Katika nchi ambayo watu wengi wanajikimu kutokana na kilimo, wastani wa asilimia 90 ya mazao yanaweza kuharibiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa iliyoathirika.” Limeongeza shirika la WFP. 

Dhoruba hizo za mfululizo zimeathiri usambazaji wa soko na uwezekano wa kupandisha bei ya chakula na kusababisha uhaba wa chakula kuongezeka katika miezi ijayo.  

"Tunachokiona nchini Madagascar ni athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi ambazo ni mfululizo wa dhoruba na ukame wa muda mrefu unaoathiri mamia kwa maelfu ya watu," amesema Brian Lander, naibu Mkurugenzi wa Dharura wa WFP. 

Ameongeza kuwa "Wakati WFP inatoa chakula muhimu baada ya dhoruba, tunahitaji pia kufikiria haraka jinsi jumuiya hizi zitakavyoweza kujenga mnepo dhidi ya ukweli huu mpya unaowakabili."