Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamia ya watu wapata chanjo ya COVID-19 katika kampeni ya chanjo ya WHO na serikali Kenya

Watu binafsi pamoja na mashirika wanahakikisha watoto wanazingatia unawaji mikono kwa mfano mama na mwana Kenya
© UNICEF/Translieu/Nyaberi
Watu binafsi pamoja na mashirika wanahakikisha watoto wanazingatia unawaji mikono kwa mfano mama na mwana Kenya

Mamia ya watu wapata chanjo ya COVID-19 katika kampeni ya chanjo ya WHO na serikali Kenya

Afya

Mamia ya watu wamejitokeza kupata chanjo ya COVID-19 katika kampeni ya chanjo ya siku 10 inayoendeshwa na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na serikali ya Kenya ikizilenga jamii ambazo mara nyingi ni vigumu kuzifikia katika kaunti 11 kati ya kaunti 47 za nchi hiyo.

Kwa mujibu wa WHO kaunti hizo 11 zinazolengwa na kampeni hiyo iliyoanza Jumanne wiki hii ( 22 Februari 2022)  zina viwango vidogo vya waliopata chanjo dhidi ya COVID-19 na ili kufanikisha lengo shirika hilo la Umoja wa Mataifa linashirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali za kaunti, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wengine kuhakikisha kwamba hakuna atakayeachwa na chanjo hiyo muhimu.

Miongoni mwa mbinu zinazotumika kuhakikisha watu wengi zaidi katika jamii wanashiriki ni kutotegemea tu watu kufika kwenye vituo vya afya, hivyo wameweka vituo vya chanjo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni, kwenye vituo vya mabasi, masokoni , kwenye bustani za kupumzika na hata makanisani. 

Na makundi yanayoshirikishwa katika kuchagiza kampeni hiyo ni pamoja na vijana, wanawake, waendesha bodaboda, viongozi wa dini na wale ambao mara kwa mara husahaulika kama vile watu wenye ulemavu. 

Awamu ya kwanza ya kampeni ilifanyika mwezi Desemba mwaka jana ambapo WHO ilitoa msaada wa kiufundi na fedha katika kaunti hizo 11. Katika siku ya kwanza ya kampeni ya sasa mfano kwenye kaunti ya Kisumu watu 321 walipatiwa chanjo kwenye kituo kilichowekwa kanisani, 132 kati yao ni watu wanaoishi na ulemavu huku wengine 189 ni wale wasio na makazi. 

Kaimu mwakilishi wa WHO nchini Kenya Dkt. Juliet Nabyonga amesema “mbali ya kufadhili kampeni za uelimishaji kuhusu hatari za COVID-19, WHO nchini humo imewekeza pia rasilimali katika kuzishirikisha jamii ili kuelewa vikwazo vinavyowakabili katika kutekeleza mikakati ya kudhibiti janga la COVID-19.”