Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongezeka kwa mashambulizi Ukraine kunaweka rehani maisha ya Watoto:UNICEF

Afina alikuwa na umri wa miaka miwili pekee wakati makombora yalipoanza kuanguka mashariki mwa Ukraine.
© UNICEF/Aleksey Filippov
Afina alikuwa na umri wa miaka miwili pekee wakati makombora yalipoanza kuanguka mashariki mwa Ukraine.

Kuongezeka kwa mashambulizi Ukraine kunaweka rehani maisha ya Watoto:UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF limesema linatiwa wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mashambulizi yaliyoanza nchini Ukraine ambayo yanatoa tishio kubwa kwa maisha na ustawi wa Watoto milioni 7.5 nchini humo. 

Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine M. Russell amesema “Milio ya silaha nzito kwenye mstari wa makabiliano tayari imeharibu miundombinu muhimu ya maji na vifaa vya elimu katika siku za hivi karibuni. Endapo mapiganio hayatopungua hivi karibuni makumi ya maelfu ya familia zinaweza kulazimika kuyahama makazi yao, na hivyo kuzidisha mahitaji ya kibinadamu.” 

Ameongeza kuwa "UNICEF inafanya kazi kote mashariki mwa Ukraine kuongeza programu za kuokoa maisha kwa watoto. Hii ni pamoja na kusafirisha huduma ya dharura ya maji salama kwenye maeneo yenye migogoro, vifaa vya muhimu vya afya, elimu, na usafi karibu iwezekanavyo kwa jamii zilizo karibu na msitari wa makabiliano na kufanya kazi na manispaa ili kuhakikisha kuna msaada wa haraka kwa watoto na familia zinazohitaji. “ 

Timu zaUNICEF za kuhamahama pia zinasaidia huduma ya kisaikolojia kwa watoto walioathirika na ukosefu wa usalama kwa muda mrefu. 

Mashirika mengine pia ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuratibu misaada ya kibinadamu OCHA yako ytayari kuendelea kuisaidia jamii ya Ukraine inayoathirika na mashambulizi hayo. Mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Ukraine Osnat Lubrani leo amesema “Tunapojaribu kuelewa kinachoendelea katika sehemu mbalimbali za nchi, nataka kueleza mshikamano wetu na watu wa Ukraine. Umoja wa Mataifa na washirika wetu wa kibinadamu wamejitolea kukaa hapa na kutoa msaada. Tuko hapa kusaidia watu waliochoshwa na migogoro ya miaka mingi na tuko tayari kuchukua hatua  iwapo kutakuwa na ongezeko lolote la mahitaji ya kibinadamu.”