Rais Putin zuia majeshi yako kuishambulia Ukraine, ipe amani fursa:UN 

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiwa katika mkutano wa dharura kuhusu Ukraine.
UN Photo/Evan Schneider
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiwa katika mkutano wa dharura kuhusu Ukraine.

Rais Putin zuia majeshi yako kuishambulia Ukraine, ipe amani fursa:UN 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemsihi Rais wa Urusi Vladimir Putin kuchagua amani badala ya vita wakati wa kikao cha dharura kuhusu Ukaraine usiku huu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani. 

Akisisitiza umuhimu wa kutoa fursa ya kutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia ya amani Guterres amesema, “Siku ya leo imeghubikwa na uvumi na dalili kwamba mashambulizi dhidi ya Ukarine yako karibu. Katika siku za hivi karibuni, kulikuwa na hali kadhaa zilizo na dalili zinazofanana, na uvumi sawa na huo. Na sikuwahi kuuamini, nikiwa na hakika kwamba hakuna jambo zito lingetokea. Nilikosea, na ningependa kutofanya makosa kama hayo tenana leo.” 

Hivyo Katibu Mkuu hakusita kuanika yaliyo moyoni mwake, “Ikiwa kweli operesheni inatayarishwa, nina jambo moja tu la kusema kutoka moyoni mwangu, Rais Putin, zuia wanajeshi wako kushaimbulia Ukraini. Ipe amani nafasi, watu wengi sana tayari wameshakufa.” 

Mkuu wa masuala ya kisiasa wa UN 

Naye msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya kisiasa Rosemary Dicarol akisistiza kilichozungumzwa na Katibu Mkuu amesema “Mapema leo, wale wanaoitwa mamlaka ya watu wa jamhuri ya Donetsk na Luhansk waliomba usaidizi wa kijeshi kutoka Shirikisho la Urusi.” 

Lakini pia leo, mamlaka ya Ukraine ilitangaza hali ya hatari nchini kote na kutangaza hatua nyingine zinazohusiana na ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na uhamasishaji wa askari wa akiba. 

Ameongeza kuwa siku nzima zimeshuhudiwa ripoti za kutatanisha za kuendelea kwa makombora mazito kwenye msitari wa mawasiliano na vifo vya raia na wanajeshi vimeripotiwa. 

Pia kuna ripoti za kulengwa mara kwa mara kwa miundombinu ya kiraia. 

Kana kwamba hiyo haitoshi Bi. Dicarol amesema “Jioni ya leo, vyombo tofauti  vya habari vinaripoti kuhusu mkusanyiko mkubwa wa kijeshi unaoendelea na safu za kijeshi kuelekea Ukraine. Shirikisho la Urusi pia limeripotiwa kufunga anga kwa ndege za kiraia karibu na mpaka na Ukraine.” 

Hata hivyo amesema Umoja wa Mataifa hauwezi kuthibitisha hata moja ya ripoti hizo.  

Lakini amesema ikiwa maendeleo haya yangethibitishwa, yangezidisha sana hali ambayo tayari ni ya hatari sana. 

Mkuu huyo wa masuala ya kisiasa ameongeza kuwa “Mamlaka ya Ukraine pia inaripoti shambulio jipya kubwa la mtandao linalolenga taasisi kadhaa za serikali na kifedha” 

Amesema “kwa nyakati tofauti Rais wa Ukraine ametoa wito wa kuendelea kwa mchakato wa kidiplomasia , naye Rais Putin pia amezungumzia kuhusu kuendelea kujihusisha katika majadiliano,Tunazichagiza juhudi hizo hata katika wakati huu wa mwisho” amesisitiza Dicarol. 

Kwa upande wa Umoja wa Mataifa amesema wafanyakazi wake bado wako Ukraine kuendelea kutoa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Ukraine. 

Hatuwezi kutabiri kitakachotokea lakini tutaendelea kusaidia 

 

“Tumejitolea kukaa na kutoa msaada. Pande zote lazima zihakikishe ulinzi na usalama wa wenzetu. Kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu pia ni muhimu.” 

Akaenda mbali zaidi na kusema “Hatuwezi kutabiri hasa kitakachotokea katika saa na siku zijazo nchini Ukraine. Kilicho bayana ni gharama kubwa isiyokubalika  ya mateso na uharibifu kwa ajili ya kuongezeka kwa mvutano.” 

Amehitimisha taarifa yake kwa kukumbusha kuwa “Watu wa Ukraine wanataka amani. Nina hakika watu wa Urusi wanataka amani. Ni lazima tufanye kila tuwezalo ili kuhakikisha amani inakuwepo.”