Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuwajengea vyoo watoto wenye ulemavu kumewaimarisha kisaikolojia : UNICEF

Watoto wakimbizi wa Syria wakiwa darasani ndani ya kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan
Photo: UNICEF Video
Watoto wakimbizi wa Syria wakiwa darasani ndani ya kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan

Kuwajengea vyoo watoto wenye ulemavu kumewaimarisha kisaikolojia : UNICEF

Msaada wa Kibinadamu

Kambi ya wakimbizi ya Za'atari nchini Jordan inakadiriwa kuwa mtoto 1 kati ya 10 ana ulemavu, na idadi hiyo huwa kubwa zaidi wakati wa dharura.

Watoto wengi ambao wamekimbia vita nchini Syria wamepata majeraha na wanahitaji msaada wa ziada, miongoni mwa changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu ni vyoo rafiki kwa hali zao na sasa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshugulikiwa watoto UNICEF linatatua changamoto hiyo.

Kambi ya wakimbizi ya Za’atari nchini Jordan inahifadhi wakimbizi wa Syria ambapo baadhi ya watoto wamezaliwa na ulemavu lakini wengine walipata kutokana na vita.

Hamza, mtoto wa miaka 11 mwenye ulemavu hali inayomfanya kutumia baiskeli ya magurudumu anasema anapenda kwenda kila mahali na baiskeli yake, ili kuwahamasisha wengine wenye ulemavu kutojifungia ndani na kuwa kama wengine wasio na ulemavu.

Sami mwenye miaka 16 naye ni mlemavu anasema changamoto kubwa ni vyoo.

“Changamoto kubwa ilikuwa vyoo, hatukuwa nacho kwenye nyumba yetu, tulikuwa tunalazimika kwenda kutumia vyoo vya jumiya. Ilikuwa ngumu kwangu kufika kule, baba yangu alilazimika kunibeba, ilinifanya nijisikie mwenye wasiwasi.”

UNICEF iliona changamoto hiyo na kuamua kujenga vyoo kwenye nyumba zilizoko ndani ya kambi hiyo lakini kwa zile zenye watoto wenye ulemavu ilienda mbali zaidi na kujenga vyoo vya kisasa ambavyo wataweza kuvitumia

Khalid ni baba yake Ahmad ambaye anasema mafundi walioajiriwa na UNICEF baada ya kumuona mtoto wake mlemavu wanafanya kazi nzuri zaidi ya ilivyotarajiwa. Anasema, "kwa mfano walitakiwa kujenga urefu wa Sentimenta 60 za mraba lakini wametengeneza ndefu zaidi ya hapo kwa ajili ya Ahmad."

Abdelmajid ni afisa wa UNICEF nchini Jordan anasema matengenezo ya vyoo si kwenye nyumba peke yake.

“UNICEF imehakikisha vituo vyote muhimu vina vyoo ambavyo ni rafiki kwa watoto wenye ulemavu na hii inamaanisha kuwa sasa watoto wanaweza kuvifikia vituo hivi ambavyo hapo awali hawakuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Watoto wengi ambao sasa wamepata hudumu hizo za usafi wamekuwa na hali nzuri ya kisaikolojia, watoto hawa hapo awali walikuwa wamejifungia, hawakuwa wakienda nje na kucheza na wengine wala kutumia huduma zote ambazo zimewekwa kambini hapa na UNICEF kwa ajili ya watoto kama ni za elimu, kujilinda na burudani. Wamebadilika kisaikolojia sasa wanafuraha”

Sasa watoto hawa wamefurahi baada ya vyoo kutengeneza kwakuwa mbali na kuwa na uwezo wa kwenda na kiti chooni pia wanaweza kunawa mikono chooni