Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wanaonyonyesha wanalengwa na makampuni ya maziwa ya kopo

Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.
© UNICEF/Zahara Abdul
Lucy Atokoru, 28 ananyonyesha mtoto wake nyumbani kwake Omugo, Wilaya ya Arua.

Wanawake wanaonyonyesha wanalengwa na makampuni ya maziwa ya kopo

Wanawake

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la afya ulimwenguni WHO na la kuhudumia watoto UNICEF na wadau wao, wametoa wito kwa serikali, wahudumu wa afya, na tasnia nzima inayohusika na vyakula vya watoto kutekeleza kikamilifu na kutii mahitaji ya Kanuni za kiafya.

Wito huo unatokana na kwamba zaidi ya nusu ya wazazi na wanawake wajawazito yaani asilimia 51 waliohojiwa kwa ajili ya ripoti mpya ya mashirika hayo mawili WHO na UNICEF, wanasema wamekuwa wakilengwa na ushawishi wa biashara kutoka kwa makampuni ya maziwa ya viwandani, ambayo mengi yanakiuka viwango vya kimataifa vya ulishaji wa watoto wachanga.  

UNICEF na WHO zinashikilia kuwa tasnia ya maziwa yenye thamani ya dola bilioni 55 inatumia mikakati ya kimasoko na isiyo ya kimaadili ili kushawishi maamuzi ya wazazi ya ulishaji wa watoto wachanga na mila za kinyonyaji zinazohatarisha lishe ya watoto na kukiuka ahadi za kimataifa.

"Ripoti hii inaonesha kwa uwazi kwamba uuzaji wa maziwa ya kopo bado unaenea kwa njia isiyokubalika, ya kupotosha na ya fujo," Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema akitaka kanuni za uuzaji wa unyonyaji "zikubaliwe na kutekelezwa kwa haraka ili kulinda afya ya watoto."

Ripoti hiyo imegunua kwamba sio tu kwamba mbinu za uuzaji za tasnia hii ya maziwa ya watoto ni pamoja na ulengaji wa mtandaoni usiodhibitiwa na vamizi, lakini pia mitandao ya ushauri iliyofadhiliwa; ilitoa matangazo na zawadi za bure kwa wafanyakazi wa afya na hivyo  kuathiri mafunzo na mapendekezo ya wafanyakazi wa afya.

Vikwazo hidi ya kunyonyesha

Ripoti inasisitiza kwamba sekta hii mara nyingi hutoa taarifa za kupotosha na zisizothibitishwa kisayansi kwa wazazi na wafanyakazi wa afya na pia inakiuka kanuni ya kimataifa ya uuzaji wa bidhaa zinazotumika badala ya maziwa ya mama – kanuni ambazo ni makubaliano ya kihistoria ya afya ya umma kulinda akina mama dhidi ya matangazo au uuzaji wa bidhaa kutoka kwa tasnia ya chakula cha watoto.

Baada ya kuwafanyia uchunguzi wazazi 8,500 na wanawake wajawazito, na wahudumu wa afya 300 duniani kote, ripoti iligundua kuwa ushawishi wa uuzaji wa maziwa ya viwandani ulifikia asilimia 84 ya wanawake wote waliohojiwa nchini Uingereza; Asilimia 92 nchini Vietnam na asilimia 97 nchini China na kuongeza uwezekano wao wa kuchagua ulishaji watoto wao kwa maziwa ya kopo au ya viwandani.

"Ujumbe wa uwongo na wa kupotosha kuhusu maziwa ya unga ni kikwazo kikubwa kwa unyonyeshaji, unyonyeshaji ambao tunajua ni bora kwa watoto wachanga na akina mama." Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell alisema.