Skip to main content

Mwongozo mpya wa WHO/ILO kuwalinda wahudumu wa afya

Muuguzi akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto mchanga katika hospitali nchini Malawi
© UNICEF/Giacomo Pirozzi
Muuguzi akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto mchanga katika hospitali nchini Malawi

Mwongozo mpya wa WHO/ILO kuwalinda wahudumu wa afya

Amani na Usalama

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo na shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na lile la kazi duniani ILO imetoa mwongozo mpya kuhusu kuendeleza na kutekeleza mipango imara ya afya na usalama kazini kwa wafanyakazi wa sekta ya afya, wakati huu janga la COVID-19 likiendelea kuwapa shinikizo kubwa wafanyakazi hao.  

Mwongozo huo mpya umepewa kaulimbiua “kuwajali wanaojali”. Akizungumzia mwongozo huo Dkt. Maria Neira, mkurugenzi wa Idara ya mazingira, mabadiliko ya tabianchi na afya, wa WHO amesema "Hata kabla ya janga la COVID-19, sekta ya afya ilikuwa ni miongoni mwa sekta hatari zaidi kufanya kazi. Ni vituo vichache tu vya huduma za afya vilivyokuwa na programu za kusimamia afya na usalama kazini. Wafanyakazi wa sekta ya afya waliteseka kutokana na maambukizo, matatizo ya mifupa na majeraha, kunyimwa haki na kunyanyaswa mahali pa kazi, uchovu wa kupindukia na athari zingine kutokana na mazingira duni ya kazi.” 

 

Mwongozo huo mpya unazichagiza nchi kuimarisha ulinzi wa wahudumu wa afya kwa kuboresha usimamizi wa kazi za afya katika ngazi zote. Kuanzia kwenye vituo vya afay, kitaifa na kikanda.

 

Muuguzi wa Afya akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 nchini Uganda
© UNICEF/Kalungi Kabuye
Muuguzi wa Afya akijiandaa kutoa chanjo ya COVID-19 nchini Uganda

Wahudumu wa afya 115,500 wamepoteza maisha kwa COVID-19

 

Katika mwongozo huo WHO na ILO wamependekeza kutekeleza mipango endelevu ya usimamizi wa afya na usalama kazini kwa wafanyakazi wa afya katika ngazi za zote.

 

Na programu hizi zinapaswa kushughulikia hatari zote za kazi ikiwemo kuambukizwa magonjwa, kiwewe, majeraha ya kimwili, athari za kemikali na kisaikolojia.

 

Wameongeza kuwa janga la COVID-19 limeongeza shinikizo zaidi kwa wafanyikazi wa afya na kuanika hatari zilizopuuzwa kwa afya zao, usalama na ustawi wao.

 

Zaidi ya kituo kimoja cha afya kati ya vitatu havina sehemu maalum za usafi kwenye maeneo ya huduma.

 

Chini ya nchi moja kati ya sita ndizo zina sera ya kitaifa ya mazingira salama ya kazi katika sekta ya afya.

 

Hatimaye, janga la COVID-19 limeainisha gharama ya ukosefu huu wa kimfumo wa dhamana kwa afya, usalama na ustawi wa wafanyikazi wa sekta ya afya.

 

"Katika miezi 18 ya kwanza ya janga hili, takriban wafanyikazi wa afya 115,500 walikufa kutokana na COVID-19," amesema James Campbell, mkurugenzi wa idara ya wafanyikazi wa afya ya WHO.

 

Zaidi ya hayo, amesema kutokuwepo kazini kutokana na magonjwa na uchovu kumeongeza uhaba wa awali wa wafanyakazi wa afya.

 

Kwa hivyo hali hiyo imedhoofisha uwezo wa mifumo ya afya kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma na kinga wakati wa majanga.

 

Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe
© ILO/KB Mpofu
Mfanyakazi wa afya akiwa katika Maaabara ya kupima COVID-19 katika hospitali ya Mlipo nchini Zimbabwe

Kupunguza ajali za kazini na likizo ya ugonjwa

 

Kwa upana zaidi, mwongozo huu pia unaeleza majukumu ambayo serikali, waajiri, wafanyakazi na huduma za afya kazini wanapaswa kutekeleza katika kulinda afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi wa afya.

 

Pia unasisitiza umuhimu wa kuendelea kwa uwekezaji na mafunzo ili kudumisha maendeleo katika utekelezaji wa programu.

 

Lakini kwa upande wa ILO, mbinu madhubuti lazima ziwekwe ili kuhakikisha ushirikiano unaoendelea kati ya waajiri, mameneja na wafanyakazi wa afya, kwa lengo la kulinda afya na usalama kazini.

 

"Wafanyakazi wa afya wanapaswa kufurahia haki zao za kazi zinazostahili, mazingira salama na yenye afya ya kazi na ulinzi wa hifadhi ya kijamii kwa ajili ya huduma za afya, kutokuwepo kwa magonjwa na majeraha yanayohusiana na kazi", amesisitiza mkurugenzi wa idara ya sera za kisekta wa ILO, Alette van Leur.

 

Kulingana na Umoja wa Mataifa, nchi ambazo zimetekeleza kikamilifu programu hizo zimeshuhudia kupungua kwa majeraha yanayohusiana na kazi na magonjwa na kushindwa kuhuduria kazini kwa sababu ya magonjwa, pamoja na maboresho katika mazingira ya kazi, tija ya kazi na wafanyakazi wengi wa afya kusalia kazini.

 

WHO na ILO zitaendelea kutoa mwongozo na usaidizi kwa nchi ili kuendeleza na kutekeleza programu za afya na usalama kazini kwa wafanyakazi wa afya.