Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sahel inakabiliwa na janga kubwa la chakula, aonya mkuu wa WFP

Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.
©FAO/Giulio Napolitano
Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.

Sahel inakabiliwa na janga kubwa la chakula, aonya mkuu wa WFP

Msaada wa Kibinadamu

Idadi ya watu walio katika hatihati ya baa la njaa katika eneo la Sahel imeongezeka karibu mara kumi katika miaka mitatu iliyopita na idadi ya watu waliokimbia makazi yao imeongezeka kwa karibu asilimia 400% wakati eneo hilo likikabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa chakula katika zaidi ya muongo mmoja, anaonya mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani- WFP, David Beasley. 

Amesema kanda hiyo inayoenda hadi kusini mwa Jangwa la Sahara kwa sasa inapitia moja ya vipindi vya ukame mbaya zaidi tangu 2011. 
“Katika kipindi cha miaka mitatu tu, idadi ya watu wanaokaribia kutumbukia katika baa la njaa imeongezeka kutoka milioni 3.6 hadi milioni 10.5 katika nchi tano  ambazo ni Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.” 

Ukosefu wa usalama, umaskini na mfumuko wa bei 

Mgogoro wa sasa unatarajiwa kuzidi miaka iliyopita kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa usalama, ongezeko la umaskini kutokana na janga la COVID-19 na ongezeko kubwa la gharama ya vyakula muhimu. 
"Huu ni mgogoro mkubwa unajitokeza mbele ya macho yetu katika eneo la Sahel," ameonya David Beasley akiwa nchini Benin, baada ya kutembelea operesheni za WFP nchini Niger na Chad. 

Akaenda mbali zaidi na kusema "Nimezungumza na familia ambazo zimepitia madhila makubwa zaidi ya unavyoweza kufikiria. Wamefukuzwa kutoka kwenye nyumba zao na vikundi vya watu wenye msimamo mkali, wakiwa wenye njaa na wakikabiliwa na ukame na wamekatishwa tamaa na athari za kiuchumi za COVID-19. Tuna uhaba wa pesa na watu hawa hawana tena matumaini”. 
Wakati mahitaji ni makubwa, rasilimali za kusaidia walio hatarini ziko chini kabisa, na hivyo kuisukuma WFP katika hali ngumu ya kuchukua kutoka kwa wale ambao wana njaa ili kulisha wale wanaoteseka zaidi amesema mkuu huyo wa WFP. 
Ameongeza kuwa “nchini Niger, kwa mfano, ukosefu wa fedha unamaanisha WFP inapunguza mgao wa chakula kwa nusu.”

Wazazi wakiweka chakula kwenye sahani tayri kuwapatia wanafunzi shuleni nchini Niger
© WFP/Evelyn Fey
Wazazi wakiweka chakula kwenye sahani tayri kuwapatia wanafunzi shuleni nchini Niger

 
Kuendeleza usaidizi muhimu wa kibinadamu  

WFP inahitaji dola za Marekani milioni 470 ili kuendelea na shughuli zake katika ukanda Sahel kwa muda wa miezi sita ijayo ambapo, licha ya mazingira magumu ya usalama, limeendelea kushirikiana na washirika wa kibinadamu kudumisha msaada wa kuokoa maisha kwa watu milioni 9.3 katika nchi tano mwaka 2021. 

WFP pia imetekeleza mipango ya kujenga mnepo wa maisha ili kusaidia familia kustawi.  
Katika kipindi cha miaka mitatu tu hadi 2021, WFP na jumuiya za wenyeji wamebadilisha ekari 270,000 za mashamba yasiyokuwa na shughuli katika nchi tano za Saheli kuwa ardhi yenye tija ya kilimo na ufugaji, na kubadilisha maisha ya zaidi ya watu milioni 2.5.

Jamii ambazo zimenufaika kutokana na shughuli za kujenga uwezo wa kustahimili hali ya maisha zinafanya vyema zaidi katika kukabiliana na janga hili la ukosefu wa chakula ambalo halijawahi kushuhudiwa kwa sababu zimewezeshwa kuzalisha chakula cha kutosha kujilisha wenyewe, kuzalisha mazao mbalimbali na mapato yao. 

Wakati huo huo, nchini Benin, tishio la mzozo unaosambaa kutoka nchi jirani za Burkina Faso na Niger hadi katika mikoa ya kaskazini ni hofu inayoendelea unaoongezeka. 

Mpango wa kulisha watoto shuleni unaofadhiliwa na serikali, unaotekelezwa kwa pamoja na WFP, unatoa chakula chenye lishe bora kwa watoto 700,000 na umekuwa na jukumu muhimu katika kuunda nafasi za kazi na kuimarisha uchumi wa ndani.