Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wavuvi wa asili Ziwa Tanganyika wapatiwa mafunzo ya kulinda mazingira

Mvuvi akiwa na samaki baada ya uvuvi ziwa Tanganyika.
UN News/Devotha Songorwa
Mvuvi akiwa na samaki baada ya uvuvi ziwa Tanganyika.

Wavuvi wa asili Ziwa Tanganyika wapatiwa mafunzo ya kulinda mazingira

Tabianchi na mazingira

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limetangaza mwaka 2022 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Uvuvi wa Kisanaa na Kilimo cha Majini, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO nchini Tanzania linatoa elimu ya utunzaji wa mazingira ya ziwa Tanganyika kwa wavuvi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida kupitia mradi wao wa Fish4ACP

FAO inatoa elimu hiyo kwa kutambua ukosefu wa elimu ya uhifadhi wa mazingira huleta madhara katika nyanja mbalimbali, madhalani baadhi ya wavuvi wanaotumia mbinu za asili bila kujali mazingira wanaweza kusababisha kupungua kwa viumbe maji na hata kukosekana kwa mazao ya uvuvi.

Miongoni mwa waliopatiwa elimu ni pamoja na Charles Rubaka ambaye ni mvuvi katika Mwalo wa Kibirizi na anasema uvuvi wa asili huchangia kuharibu mazingira yanayozunguka Ziwa Tanganyika.

“Shughuli hizi tumefanya sana za utunzaji wa mwalo hususan masuala ya usafi na kuokota takataka. Lakini katika kufanya kazi hizi kuna changamoto. Mwambao huu wa ziwa letu hakuna shughuli za kilimo cha mazao na bustani maana hizo ndio zingeweza kuharibu ziwa letu, isipokuwa shughuli zinazo haribu mazingira ni takataka zinazoletwa kutoka juu.” Amesema Rubaka.

Mbali na hayo Charles akaiomba serikali kuweka mikakati thabiti ya uhifadhi wa mazingira wakati wote. “Kama serikali itatengeneza mipango rasmi ya kuzuia takataka za chupa na nyinginezo ambazo zinakuja kuharibu sehemu ya mazalia ya samaki nadhani viumbe wadogo wadogo watapata sehemu ya kuzaliana kama ilivyokuwa zamani.”

Safi Mwisigalo mfanya biashara katika Mwalo wa Kibirizi anaeleza wanavyoshiriki katika utunzani wa mazingira. “Mimi ni mkazi wa maeneo haya tunajitahidi sana kutunza mazingira sababu huwa tunapewa elimu, tunaambiwa tusifulie ziwani, tusiongee ziwani, maana samaki wanazalia pembeni ya ziwa.”

Afisa Uvuvi Halmashauri ya Kigoma UJiji, Malick Kibetele anaeleza namna serikali inaboresha miongombinu ya uvuvo.

"Katika halmashauri ya wilaya ya Kigoma ujiji tuna mialo minne, na tuna miundombinu ya kuchakata mazao ya uvuvi, tuna ghala kwa ajili ya kuhifadhia mazao ya uvuvi na wafanyabiashara wanaopeleka mazao nje ya nchi wanatumia miundombinu hii kwa ajili ya kuhifadhi mali zao”.