Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Niger yahitaji msaada wa kimataifa; wakimbizi ni wengi: UNHCR na IOM

Wahamiaji wakisajiliwa katika Kituo cha Usafiri cha Agadez nchini Niger.
IOM
Wahamiaji wakisajiliwa katika Kituo cha Usafiri cha Agadez nchini Niger.

Niger yahitaji msaada wa kimataifa; wakimbizi ni wengi: UNHCR na IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuisaidia Niger ambayo kwa sasa inahifadhi wakimbizi 250,000 kutoka nchi jirani huku ikiwa pia na wakimbizi wa ndani zaidi 250,000.

Wito huo umetolewa  na Filipo Grandi Mkuu wa UNHCR na Antonio Vitorino Mkuu wa IOM wakiwa ziarani Niger kujionea hali halisi ya wakimbizi na changamoto za uhamiaji. 

Wakiwa katika mji wa mpakani wa Oualaam wiki hii ambao unapakana na Mali na Burkina Faso viongozi hao wawili wa Umoja wa Mataifa wamesema mji huo ni maskani ya maelfu ya wakimbizi wa ndani lakini pia wakimbizi kutoka nchi jirani ya Mali ambao wameishi pamoja kwa miaka mingi. Akielezea kuhusu ziara yao Bwana Grandi anasema, "tumetumia siku nzima na mkurugenzi mkuu wa IOM hap ana tumesikia shuhuda nyungi tulipozuru miradi mbalimbali inayofadhiliwa na mashirika yetu mawili.Tumeshuhudia wanawake wakulima na kuzungumza nao.” 

Mmoja wa wanawake hao wakulima ambaye ni mkimbizi kutoka Mali alipoulizwa ajifunza wapi kilimo amesema “nilianza kujifunza ujuzi wa kilimo nyumbani nchini Mali” 

Mashirika hayo yanaendesha miradi kadhaa ikiwemo kilimo cha bustani, ujenzi wa nyumba, ubunifu  na miradi mingine kadha wa kadha inayowaletea watu hawa kipato lengo likiwa ni kuwafaidisha wakimbizi na jamii zinazowahifadhi ili waishi pamoja kwa amani. 

IOM na UNHCR wamasema watu wote hawa walifungasha virago na kuishia hapa sababu ya kukosa amani na usalama.  

Na kuongeza kuwa taifa hilo kuwa na wakimbizi wake wa ndani zaidi ya lakini mbili na nusu na kuhifadhi wakimbizi wengine kutoka nje laki mbili na nusu ni mzigo mkubwa sana lisiloweza kuubeba japo linajitahidi, hivyo wametoa wito kwa juhudi za kimataifa kuingilia kati kulisaidia taifa hilo.

“Bila juhudi za kuingilia kati tunahatarisha kurejea kwenye machafuko, tunahatarisha kuzuka tena kwa mivutano na taifa hili na ukanda huu kwa hakika hautaki hali hiyo,” amesema Grandi.