Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za kuijenga upya Haiti baada ya tetemeko la ardhi miezi 6 iliyopita 

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed akihutubia tukio la kuisaidia Haiti kujijenga upya baada ya tetemeko la ardhi lililoipiga nchi hiyo mwezi Agosti 2021.
UNDP/Borja Lopetegui Gonzalez
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina Mohammed akihutubia tukio la kuisaidia Haiti kujijenga upya baada ya tetemeko la ardhi lililoipiga nchi hiyo mwezi Agosti 2021.

Harakati za kuijenga upya Haiti baada ya tetemeko la ardhi miezi 6 iliyopita 

Msaada wa Kibinadamu

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed, yuko katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince kushiriki, Jumatano hii, katika tukio la Kimataifa la Ufadhili wa Ujenzi wa Peninsula ya Kusini mwa nchi hiyo.

Miezi sita baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea kusini magharibi mwa Haiti, ambalo lilisababisha vifo vya watu 2,200 na kujeruhi 12,700, jumuiya ya kimataifa inaungana na serikali ya Haiti kukusanya dola za Marekani bilioni 2 kwa ajili ya kurekebisha hali kwa muda mrefu. 

Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa, Haiti kwa mara nyingine iko kwenye ‘njia panda’, miezi sita baada ya tetemeko kubwa la ardhi kupiga kusini-magharibi mwa nchi hiyo na "huu sio wakati wa kukata tamaa", amesema, "kwa sababu watu wa Haiti hawakati tamaa. Mara kwa mara, wao huomboleza, kisha wanajiinua na kurejesha maisha yao,” akaongeza “Haiti iko tena kwenye njia panda. Miaka ya uwekezaji katika utulivu na maendeleo lazima ilindwe. Na taasisi za kitaifa ziko tayari kuongoza." 

Mkutano huo unalenga kukusanya fedha za kuisaidia Haiti miezi sita baada ya tetemeko la ardhi kupiga eneo hilo Agosti mwaka jana. Amina Mohammed atakutana na maafisa wa serikali wa kisiwa hicho cha Karibea, maafisa wa Umoja wa Mataifa na washirika wengine. 

Tweet URL

Uchaguzi 

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, huu ni wakati muhimu kwa Haiti, ambayo pamoja na kupata nafuu baada ya  tetemeko la ardhi, bado inatafuta njia kuelekea uchaguzi, utulivu na maendeleo endelevu. 

Amina Mohammed pia atatumia fursa ya ziara yake kisiwani humo kufanya mikutano kuhusu maendeleo katika vita dhidi ya kipindupindu na anatarajiwa kukaa kisiwani humo hadi kesho Alhamis.  

Serikali ya Haiti inakadiria kuwa dola bilioni 2 zinahitajika ili kujenga upya maeneo yote yaliyokumbwa na tetemeko la ardhi. Kati ya jumla hiyo, Dola za Marekani bilioni 1.5 zitatengwa kwa ajili ya huduma za kijamii, zikiwemo programu za makazi, afya, elimu na usalama wa chakula. 

Kuhusu kilichotokea baada ya tetemeko na hatua zilizochukuliwa  

Muda mfupi baada ya tetemeko la ardhi, serikali, Umoja wa Mataifa na washirika wengine walianza kutoa msaada wa dharura wa kibinadamu. Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya misaada ya dharura, OCHA, ilichukua jukumu kuu katika kuratibu hatua za haraka. Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, lilitoa makazi ya muda kwa watu walioachwa bila makazi, pamoja na chakula na vitu vingine muhimu. 

Shule zimefunguliwa nchini Haiti na watoto wananufaika na mgao wa chakula shuleni unaowezeshwa na WFP, Haiti na Canada.
WFP/Alexis Masciarelli
Shule zimefunguliwa nchini Haiti na watoto wananufaika na mgao wa chakula shuleni unaowezeshwa na WFP, Haiti na Canada.

 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, lilisambaza chakula kwa watoto wenye umri wa kwenda shule, njia ya kuwatia moyo kuendelea kuhudhuria masomo katika taasisi za elimu ambazo hazijaharibiwa. Takriban vituo 60 vya afya pia viliharibiwa, hivyo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu, UNFPA, waliunda wodi za dharura. Wanawake wajawazito walipata huduma na mara nyingi walijifungua kwenye mahema. 

Miezi sita baada ya tetemeko la ardhi, Haiti imepita awamu ya dharura na inalenga kupona kwa muda mrefu. Mnamo Novemba, serikali ilichapisha uchunguzi wa kiasi kinachohitajika kujenga upya eneo lililoathiriwa, takribani dola bilioni 2. Kati ya jumla hiyo, Dola za Marekani bilioni 1.5 zitatengwa kwa ajili ya huduma za kijamii, zikiwemo programu za makazi, afya, elimu na uhakika wa chakula. Mengine yatatumika katika kuboresha kilimo, biashara na viwanda na pia kukarabati huduma muhimu za miundombinu. Mipango ya mazingira pia itazingatiwa. 

Ni mambo gani dunia inajifunza kutokana na majanga ya asili? 

Haiti tayari ina uzoefu na majanga ya asili ikiwa ni pamoja na tetemeko la ardhi la Januari 12, 2010, ambalo liliua watu 220,000 akiwemo Naibu Mkuu wa Misheni ya Umoja wa Mataifa, Mbrazili Luiz Carlos da Costa. Vifo vingi vilitokea katika mji mkuu wa Port-au-Prince na maeneo ya karibu. Funzo kubwa kutokana na janga hilo lilikuwa kwamba uongozi wa kitaifa ni muhimu. 

Mnamo mwaka wa 2010, serikali ya Haiti iliathiriwa moja kwa moja na maafa na haikuwa tayari kuratibu mwitikio mkubwa wa dharura. Haiti pia inahitaji kuboreshwa ili kuanzisha hatua madhubuti zaidi za kupunguza hatari za maafa. 

Wanawake wakiwa wameungana na juhudi za jamii kurekebisha barabara ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi lililopiga eneo la kusini-magharibi mwa Haiti.
WFP Haiti/Theresa Piorr
Wanawake wakiwa wameungana na juhudi za jamii kurekebisha barabara ambazo ziliharibiwa na tetemeko la ardhi lililopiga eneo la kusini-magharibi mwa Haiti.

 

Je, Haiti inakumbana na matatizo gani mengine? 

Tetemeko la ardhi la 2021 lilitokea wakati nchi ilikuwa inakabiliwa na migogoro mingi, ya kiuchumi, kisiasa, usalama, kibinadamu na maendeleo. Haiti ina kiwango cha juu cha umaskini na inashika nafasi ya 170 katika orodha ya mataifa 189 duniani iliyowasilishwa katika Ripoti ya Maendeleo ya Binadamu 2020, ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP. Uchumi uko matatani, huku watu waliojihami kwa silaha hivi karibuni wakizuia usambazaji wa mafuta, hali ambayo karibu imeifanya nchi hiyo kusimama. Ukosefu wa usalama, utekaji nyara na magenge yanayodhibiti vitongoji kadhaa katika mji mkuu wa Port-au-Prince. Mnamo Julai 2021, Rais wa Haiti, Jovenel Moise, aliuawa ndani ya nyumba yake na uchunguzi unaendelea. Mbali na haya yote, pia Haiti inakabiliwa na tishio la Covid-19.  

Je, Haiti inawezaje kupona kutokana na janga hili la hivi punde? 

Leo Februari 16, serikali imeandaa mkutano wa kimataifa huko Port-au-Prince kwa lengo la kukusanya angalau dola bilioni 1.6 kati ya bilioni 2 zinazohitajika ili kurejesha nchi kwenye mstari baada ya tetemeko la ardhi. 

Ombi hili linakuja wakati ambapo nchi nyingi wafadhili kote ulimwenguni zinakabiliwa na athari za kifedha kutokana na janga la Covid-19. 

Aidha, Haiti inashindania ufadhili na majanga mengine ya sasa kama vile Afghanistan na eneo la Tigray nchini Ethiopia. Wahaiti wakubwa wanaoishi nje ya nchi, hasa Marekani, wanaweza kuwa rasilimali kwa Haiti, kwa matarajio kwamba jumuiya hizi zitasaidia ufadhili. Mashirika ya hisani ya Marekani pia yanalengwa. 

Jumuiya ya kimataifa nchini Haiti tayari imeonywa kwamba iwapo nchi hiyo haitapata usaidizi unaohitajika, ahueni yake, maendeleo yake na uwezo wake wa kukabiliana na majanga ya asili vitaathiriwa vibaya.