Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujumusha watu wenye ulemavu ni muarobaini wa kutomwacha yeyote nyuma- Guterres

Rafael Salafranca anapigia chepuo matumizi ya barakao zinazoonesha mdomo ili kuondoa kikwazo cha mawasiliano na viziwi
Viendo Tentiendo
Rafael Salafranca anapigia chepuo matumizi ya barakao zinazoonesha mdomo ili kuondoa kikwazo cha mawasiliano na viziwi

Kujumusha watu wenye ulemavu ni muarobaini wa kutomwacha yeyote nyuma- Guterres

Haki za binadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amehutubia mkutano wa pili wa kimataifa kuhusu watu wenye ulemavu na kutaja vipaumbele vitatu ambavyo anaona ni muhimu ili kuhakikisha kuwa haki za kundi hilo haziachwi nyuma hasa wakati huu dunia inapitia changamoto za kiafya, kiuchumi na kimazingira.

Ametaja vipaumbele hivyo kuwa ni kuhakikisha maendeleo yanazingatia watu wenye ulemavu na jumuishi, pili ushirikiano wa dhati na mpana wa kujumuisha watu wenye ulemavu kufanikisha ajenda 2030 ya maendeleo endelevu na tatu watu wenyewe wenye ulemavu hususan wanawake washike usukani kwenye uongozi katika ngazi mbalimbali.

Katibu Mkuu amewaeleza washiriki wa mkutano huo wa siku mbili unaofanyika kwa njia ya mtandao kuwa vipaumbele hivyo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 limezidi kupanua pengo la ukosefu wa usawa unaokabili watu wenye ulemavu.

Majanga ni mwiba wa pili kwa watu wenye ulemavu

“Shule zinapofungwa, wanafunzi wengi wenye  ulemavu wanaenguliwa kwa kukosa teknolojia na vifaa saidizi vya kuwawezesha kusomea majumbani. Wafanyakazi wenye ulemavu nao halikadhalika, wao mara nyingi ndio wa kwanza kupoteza kazi na wa mwisho kuajiriwa upya. Wanawake na wasichana wenye ulemavu ambao tayari wanakabiliwa na ubaguzi, wanakuwa hatarini zaidi kukumbwa na ukatili na unyanyasaji,” amesema Guterres.
Katibu Mkuu amesema miaka miwili iliyopita imedhihirisha kwa uchungu umuhimu wa dharura kwa “sote kushirikiana ili kusongesha haki za watu wenye ulemavu duniani kote. Mwaka 2018 serikali na mashirika duniani walikutana na kupitisha ahadi za kiwango cha juu za kitaifa na kimataifa kwa ujumuishaji wa watu wenye ulemavu.”

Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) akishiriki mkutano wa kimataifa wa watu wenye ulemavu.
UN / Evan Schneider
Katibu Mkuu wa UN António Guterres (kushoto) akishiriki mkutano wa kimataifa wa watu wenye ulemavu.

Ni kwa msingi huo amesema kuwa mkutano wa sasa unatoa fursa ya kutathmini jitihada zilizofanyika na yeye anaona vipaumbele hivyo vitatu.

Akivichambua Guterres amesema kipaumbele cha kwanza cha maendelo yanayojumuisha zaidi watu wenye ulemavu kinamulika uzingatiaji wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye juhudi za maendeleo. “Kila mtu kokote aliko anapaswa kuwa huru kwenda shule, hospitali au kuanza familia yake bila kikwazo chochote.”
Kipaumbele cha pili ni kupanua kwa dhati wigo wa ushirikiano akisema “ni kwa kufanya kazi pamoja kuanzia serikali, mashirika ya kimataifa , mashirika ya kiraia na sekta binafsi ndipo tunaweza kutekeleza mkataba wa kimataifa wa watu wenye ulemavu na kufanikisha ajenda 2030 kwa maendeleo endelevu kwa watu wenye ulemavu.”

Na kipaumbele cha tatu ni ujumuishaji wa wanawake wenye ulemavu katika juhudi zote kuanzia uongozi hadi utekelezaji wa mipango akisema “lazima tuzingatie wito wa watu wenye ulemavu ya kwamba ‘hakuna chochote kuhusu sisi bila kutujumuisha sisi.”

Mkutano huu umeandaliwa kwa pamoja na Ushirikiano wa watu wenye ulemavu duniani, serikali ya Norway na Ghana.