Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

KWA UFUPI: Kutoka UNFPA na IOM Tanzania

UNFPA nchini Tanzania imelipatia dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi nchini humo pikipiki 10 kwa lengo la kusaidia harakati za kutokomeza ukatili wa kijinsia na vitendo vingine viovu kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.
UNFPA/ Warren Bright
UNFPA nchini Tanzania imelipatia dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi nchini humo pikipiki 10 kwa lengo la kusaidia harakati za kutokomeza ukatili wa kijinsia na vitendo vingine viovu kama vile ukeketaji na ndoa za utotoni.

KWA UFUPI: Kutoka UNFPA na IOM Tanzania

Haki za binadamu

Nchini Tanzania hii leo mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA na lile la uhamiaji, IOM yametekeleza masuala tofauti ikiwemo haki za binadamu na  uhamiaji.

UNFPA na pikipiki kwa jeshi la polisi:

Tweet URL

Nchini Tanzania hii leo shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na masuala ya afya ya uzazi, UNFPA limekabidhi pikipiki 10 kwa dawati la jinsia na watoto la jeshi la polisi nchini humo kwa lengo la kulinda kila mwanamke na mtoto wa kike dhidi ya ukatili wa kijinsia na vitendo viovu kama vile ndoa za utotoni na ukeketaji.

Pikipiki hizo zimekabidhiwa na Afisa Mtendaji wa UNFPA Tanzania Georgette Kyomba kwa Mkuu wa jeshi la polisi nchini Tanzania Inspekta Jenerali Simon Sirro ambaye ametoa wito kwa watendaji wa polisi watakaopokea pikipiki hizo katika mikoa husika wazitumie kwa ajili ya kutokomeza ukatili wa kingono na kijinsia.

Kwa upande wake Bi. Kyomba amesema UNFPA imejizatiti kulinda kila mwanamke na kila mtoto wa kike dhidi ya ukatili wa kingono na kijinsia sambamba na vitendo vingine viovu kama vile ndoa za utotoni na ukeketeji au FGM.

IOM na kusafirisha wakimbizi wa DRC kuelekea Marekani

Tweet URL

Na tukitamatishia huko huko Tanzania,  shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM limefanikisha mpango wa kuhamishia wakimbizi kwenda nchi ya tatu ambapo wakimbizi 57 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC waliokuwa wanaishi katika kambi ya wakimbizi huko Kasulu mkoani Kigoma wameondoka kwenda Marekani.

Kupitia mtandao wake wa Twitter, Mkuu wa IOM nchini Tanzania Dkt. Qasim Sufi amesema wakimbizi hao wameondoka jana tarehe 15 mwezi huu wa Februari na kwamba mpango huo wa kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu ni moja ya vipengele vikuu vitatu vya kusaka suluhu ya kudumu kwa wakimbizi.

Amesisitiza kuwa usaidizi kwa wakimbizi kuhamia nchi ya tatu ni bure na kwamba iwapo mtu yeyote analaghaiwa ili alipe gharama basi atoe ripoti kupitia anwani pepe fraudiomtanzania@iom.int.