Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Redio Kwizera: Kutoka kuhudumia wakimbizi kutoka Rwanda hadi mikoa mitano Tanzania  

Redio za zamani zikioneshwa katika jumba la makumbusho la Chihuly, Seattle, USA.
Unsplash/Rod Flores
Redio za zamani zikioneshwa katika jumba la makumbusho la Chihuly, Seattle, USA.

Redio Kwizera: Kutoka kuhudumia wakimbizi kutoka Rwanda hadi mikoa mitano Tanzania  

Wahamiaji na Wakimbizi

Redio Kwizera ya wilayani Ngara mkoani Kagera Tanzania, tangu mwaka 1995 ilipoanzishwa na huduma ya majesuit wa kikatoliki kwa wakimbizi (JRS) kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, ikiwa ni hatua ya kutaka kuwasaidia wakimbizi kukutana na wapendwa wao waliopoteana nao wakati wa kukimbia vita ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994, imeendelea kuwa msaada kwa wakimbizi na wenyeji.  

Peter Lusaya ambaye ni Afisa Uzalishaji wa vipindi wa Redio Kwizera na Swaum Juma ambaye ni Mwandishi na Mtayarishaji vipindi wanaeleza kinagaubaga kuhusu historia na shughuli ambazo zinafanywa na kituo hicho. 

“Kihistoria redio Kwizera ilianzishwa mwaka 1995,” ndivyo anavyoanza kueleza Bwana Lusaya na kisha anaendelea, “na alianza wakati ule ambapo kulikuwa na wimbi na wakimbizi kutoka Rwanda kutokana na mauaji yaliyotokea mwaka 1994 ambapo katika wilaya hii ya Ngara katika eneo la Benako, kulikuwa na wakimbizi zaidi ya laki nane katika eneo lile dogo. Kwa hivyo na mahitaji yaliyokuwa pale ni makubwa, hivyo shirika la Majesuit wa kaniasa katoliki likaja pale kutoa huduma za kuweza kutia taarifa ya watu ambao wamepotelewa na wenzao. Lengo lilikuwa ni kuunganisha watu waliopotelewa. Wakati huo basi hakukuwa na namna nyingine ya kuweza kuwasiliana zaidi ya kutumia njia hiyo kwa kuwa hakukuwa na redio kipindi hicho. Utakumbuka hata tekonolojia ya simu za mkononi haikuwepo.” 

Walikuwa wanatumia matangazo kwenye gari  

Bwana Lusaya anaeleza kuwa kabla ya kuanzisha kituo cha redio, Majesuit wa kikatoliki walikuwa wanatumia gari lenye vipaza sauti na spika kuzunguka katika maeneo mbalimbali kutangaza watotot waliopotea na ndugu ambao walikuwa wanahitaji misaada ya namna mbalimbali lakini pia kuwapa taarifa mbalimbali watu kuhusu matukio kwa kadri yalivyokuwa yanatokea. 

Assumpta Massoi/UNNewsKiswahili
Habari za UN- Redio Kwizera ya Ngara Tanzania yaendelea kujiaminisha

Kutoka wilaya 1 hadi mikoa mitano 

Hivi sasa redio Kwizera imevuka mipaka ya eneo dogo la Ngara ambako ilikuwa inawahudumia wakimbizi na wenyeji wachache, na sasa inasikika katika mikoa mitano yaani Mwanza, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Geita. “Kwa hiyo redio imeendelea kupanuka na kuaminiwa.” Anaeleza Bwana Lusaya. 

Ushirikiano na UNHCR 

Redio Kwizera imekuwa ikishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi kwa namna mmbalimbali lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha redio hiyo inakuwa na uwezo wa kuwafikishia ujumbe wakimbizi. “Na kwa hivyo ushirikiano huu umekuwa na manufaa makubwa.” Anasema Afisa uzalishaji vipindi.   

Pia UNHCR imeakuwa ikiisaidia redio hiyo vifaa mbalimbali na pia kuishirikisha redio katika masuala mbalimbali kwa ajili ya kuwafikishia ujumbe wakimbizi na jamii nyingine mbalimbali. 

Soundcloud

Kwizera na Covid-19 

Kituo hiki cha redio Kwizera kimekuwa na manufaa makubwa wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 kwani wakati shule zilipofungwa, kilikuwa kinarusha matangazo ya masomo na hivyo wanafunzi wakawa wanasoma kwa njia ya redio wakiwa nyumbani. 

Tweet URL

Naye Swaum Juma ambaye ni Mwandishi wa habari na mtayarishaji wa vipindi wa kituo hicho cha redio Kwizera anasema kuna faida kubwa ambazo kituo hicho cha redio kimeleta, mathalani anasema, “tuna kipindi ambacho tunakiita jirani ni ndugu ambacho kinahusisha zaidi wale watu ambao wako kwenye zile kambi za wakimbizi na walioko nje ya kambi. Mfano kwa Kibondo na Kasulu Kigoma. Hii ni kusaidi jamii ambazo zinaishi nje ya kambi na ndani ya kambi kuishi kama ndugu na kuhamasisha amani na kuishi bila migogoro.” 

Mazingira 

Swaum anaeleza kuwa kipindi cha mazingira kimesaidia jamioi ya wakimbizi na wenyeji katika kutunza mazingira. Kwa mfano kuna maeneo ambayo kulikuwa na wakimbizi wakaondoka, lakini wakati wakiishi maeneo hayo mazingira yaliharibika pengine kutokana na kukatwa kwa miti kwa ajili ya shughuli mbalimbali. “Kwa hiyo kupitia kipindi hicho cha mazingira kimechangia kuhamasisha jamii ya wakimbizi pamoja na wenyeji kuhakikisha wanatunza mazingira.”  Anahitimisha Swaum.