Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na serikali ya Japan kuwanusuru walioathirika na Tsunami na volcano Tonga 

Mlipuko wa volkano na Tsunami ya Tonga umeweka wazi mazingira hatarishi ya visiwa vidogo na Mataifa yanayoendelea (SIDS).
© Konionia Mafileo
Mlipuko wa volkano na Tsunami ya Tonga umeweka wazi mazingira hatarishi ya visiwa vidogo na Mataifa yanayoendelea (SIDS).

UNICEF na serikali ya Japan kuwanusuru walioathirika na Tsunami na volcano Tonga 

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na serikali ya Japani wametangaza ushirikiano mpya wa kuchangia dola milioni 1.25 kuisaidia serikali ya Ufalme wa Tonga kuhakikisha kuwa takriban watu 19,250 wakiwemo watoto 10,000 walioathiriwa na mlipuko wa volcano na tsunami hivi karibuni wanapata maji safi ya kutosha ya kunywa, mazingira safi , pamoja na afya njema. 

Ahadi hii inadhihirisha kuendelea kwa ushirikiano thabiti kati ya watu wa Japan na shirika la UNICEF unaolenga kuboresha maisha ya watoto wote wanaoishi katika ukanda wa Pasifiki. 

Akizungumzia msaada huo Balozi mdogo wa Japan kwenye Ufalme wa Tonga, Bwana Munenaga Kensaku amesema, “milipuko mikubwa ya volkano na tsunami imeathiri kwa kiasi kikubwa kisiwa cha Tonga, na maelfu ya watu bado wanaendelea kuathiriwa na kuteseka. Wakati watu na nserikali ya Tonga wamekuwa wakijitahidi kuondokana na matatizo yaliyosababishwa na majanga hayo, Tonga ikambukizwa na janga la COVID-19 kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili kuwa huru bila maambukizi ya COVID-19, "  

Balozi huyo ameongeza kuwa, “msaada huu utasaidia Tonga kuharakisha juhudi zao za kujikwamua kutoka kwa janga hili na pia kupambana na COVID-19. Ninaamini Tonga itashinda majanga haya ya mlipuko wa volkano na Tsunami na pia janga  la COVID-19.” 

Kwa mujibu wa UNICEF mlipuko wa volcano ya chini ya maji ya Hunga Tonga Hunga Ha’apai umesababisha uharibifu wa miundombinu muhimu ya maji, huduma za usafi wa mazingira na usafi (WASH) na kukatizwa kwa huduma kwa familia, shule na vituo vya afya.  

Shirika hilo limesisitiza kuwa, “hali hii imezidi kuwaweka watu kwenye hatari ya kupata magonjwa kutokana na kunywa maji yasiyo salama, kujisaidia haja kubwa kwenye maeneo ya wazi, na kushindwa kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka."