Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kujaa maji kwa ziwa Albert Uganda kwazidi kuleta zahma, UNHCR yaingilia kati

Nyanjura Nyangoma akiwa na familia ya watu 14 akiwaza na kuwazua juu ya mustakabali wao baada ya mafuriko katika Ziwa Albert kuwalazimu kukimbia makwao.
UN/ John Kibego
Nyanjura Nyangoma akiwa na familia ya watu 14 akiwaza na kuwazua juu ya mustakabali wao baada ya mafuriko katika Ziwa Albert kuwalazimu kukimbia makwao.

Kujaa maji kwa ziwa Albert Uganda kwazidi kuleta zahma, UNHCR yaingilia kati

Tabianchi na mazingira

Nchini Uganda, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR limesaidia wananchi walioathiriwa na kujaa kwa maji katika Ziwa Albert, eneo mafuriko ambayo yana historia tangu mwaka 1962. Watu 100,000 wamelazimika kukimbia makazi  yao huku shughuli za kibiashara na kijamii zikiathirika.
 

 

Kiwanda hiki cha samaki cha Butyaba kimefungwa baada ya kutwama kwenye maji yatokanayo na ongezeko la maji katika Ziwa Albert.
UN/ John Kibego
Kiwanda hiki cha samaki cha Butyaba kimefungwa baada ya kutwama kwenye maji yatokanayo na ongezeko la maji katika Ziwa Albert.

Katika ufukwe wa Kibiro wilayani Hoima nchini Uganda, mafuriko yanasababisha upepo mkali ziwani ambapo Nyanjura Nyangoma mmoja wa manusura anasema nyumba yake yote imezama kwenye maji.
 
Kilomita 15 kutoka ufukwe wa Kibiro ni ufukwe wa Butyaba ulio mkubwa zaidi kuliko yote kwenye Ziwa Albert. Kuna majengo ya kiwanda cha samaki yaliogharimu takribani dola milioni 1.1 na sasa yametwama.  

 Pia kuna hospitali ya serikali ya iliyogharimu karibu dola 250,000 za ujenzi na sasa iko katika hali ya kutotumika tena. 
 
Mafuriko haya ya kihistoria yalianza kama mzaha mwanzoni mwa mwaka 2020 hasa kwa watoto na vijana. Serikali ilikutwa ikikipambana kutokomeza janga la nzige huku COVID-19 ikisogelea. Ingawa tishio la nzige halipo tena, haieleweki ni lini na vipi majanga ya mafuriko na COVID-19 yatakwisha. 

Jasmin Majjid akiwa amesimama mbele ya nyumba yake ambayo alitumia takribani dola 1,700 kuinusuru lakini ilishindikana.
UN/ John Kibego
Jasmin Majjid akiwa amesimama mbele ya nyumba yake ambayo alitumia takribani dola 1,700 kuinusuru lakini ilishindikana.

Alipokuwa bado ana matumaini, Bi Jasmini Majid alijaribu kuziba maji akisema alipoteza takribani dola 1,700 akijaribu kuzuia maji lakini haikuwezekana.
 
Mafuriko kama haya yaliwahi kushuhudiwa mwaka 1962 ambapo mzee Baranaba Bagadira Kakura wa Waseko wilayani Buliisa ni shuhuda. Anasema mafuriko yalifukuza watu wote na wakakimbilia barabarani na zaidi ya yote waathirika wakuu wamekuwa ni wahamiaji waliopuuza onyo la wazee kutoingilia maeneo haya. 

Alizaliwa mwaka 1962 wakati wa mafuriko na kupewa jina la shida

Naye Kabonesa Nyansonga alizaliwa siku ya kuanza kwa mafuriko ya mwaka 1962. Anasema upepo ulikuwa mkali na kwa sababu ya maji mengi mama yake alikimbilia sehemu ya muinuko na alijifungua kwa shida na ndipo akampatia jina Kabonesa likimaanisha shida.
 
Miaka sitini badaye yametokea tena na kukosesha makaazi watu wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 100,000. Serikali imetoa msaada ikishirikiana na wadau wake lakini ni wachache waliofikiwa. 

 

Kabonesa Nyasonga ni mkazi wa Butyaba, alipatiwa jina hilo kwa sababu alizaliwa mwaka 1962 wakati wa mafuriko ya kwanza ya Ziwa hilo na wakati mama yake alijifungua alipata shida kubwa na ndipo akampatia jina Kabonesa maana yake shida.
UN/ John Kibego
Kabonesa Nyasonga ni mkazi wa Butyaba, alipatiwa jina hilo kwa sababu alizaliwa mwaka 1962 wakati wa mafuriko ya kwanza ya Ziwa hilo na wakati mama yake alijifungua alipata shida kubwa na ndipo akampatia jina Kabonesa maana yake shida.

Simon Bimbona ni mkuu wa wahudumu wa umma wilayani Buliisa na anasema. “Ofisi ya waziri mkuu pia ilitupatia mahema, maharagwe na unga wa mahinidi tulivyogawa katika sehemu za Butyaba na Buliisa. Kwa hiyo LACWADO nao wanapojitokeza kutusaidia tunashukuru sana kwani wao ni wadau wetu wa maendeleo. Bila shaka msaada wa dharura hautoshi kwa sababu ni wachache wanaopokea. Nji endelevu ni kuhakikisha watu hawavunjiki moyo. Msaada ni wa siku moja au mbili na kwa hivyo ni muhimu tujitahidi kupata njia endelevu tuone jinsi gani wanaweza kuishi baada ya kipindi hiki” 

Soundcloud

Hali kama hii imeshuhudiwa kwenye maeneo mengine oevu ingawa kwa viwango tofauti. Bashir Bijaju anaamii serikali ina uwezo wa kusaidia wote. 
 
Serikali ya Uganda ilitangaza  inabuni mpango maalumu wa kupatia makaazi wakimbizi hawa wa tabianchi.  Mary Grace Mugasa ni Niabu Waziri wa huduma za umma na anasema, “wajibu wa seerikali kutoa msaada wa dharura kwa watu hao kupitia mfuko a dharura. Lakini unakuta kwamba fedha ambazo zingesaidia katika sekta za elimu na afay kwa mfaa zinaelekezwa kusaidia waaliofurushwa makawo na mafuriko. Hivyo tunakuwa na uhaba wa rasilimali” 

Kituo cha afya cha Butyaba nchini Uganda kimetwama kwenye maji kutokana na ongezeko la maji kwenye ziwa Albert.
UN/ John Kibego
Kituo cha afya cha Butyaba nchini Uganda kimetwama kwenye maji kutokana na ongezeko la maji kwenye ziwa Albert.

UNHCR yaitikia wito wa kusaidia

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi la UNHCR limeitikia hali hii ikizingatiwa kuwa Uganda inahifahdi wakimbizi zaidi ya milioni moja. 

Wendy Daphine  Kasujja ni naibu afisa wa mawasiliano UNHCR, Uganda na anasema“serikali ya Uganda ilifika ofisi ya UNHCR ikiomba msaada wa kibinadamu. UNHCR iliitikia kwa kutoa kile kiitwacho msaada usio wa chakula ambao ni pamoja na mahema, vyandarua, mablanketi, ndoo na mapanga ili kuwawezesha kujenga makaazi ya muda ya waliopoteza makaazi” 
 
Wamefikisha msaada kwa watu zaidi ya 10,000 wilayani Ntoroko na Bundibugyo akifafanua kuwa “Katika uitikio huo tulifanikiwa kufikisha msaada kwa kaya 3,000 zenye watu wapatao 14,000” 
 
Na kuahidi kuwa “kati ya ongezeko la mabadiliko ya tabianchi na athri zake kwa binadamu, UNHCR itaendelea kuhsirikiana na serikali kutoa msaada kila itakapoitishwa na ikabainika kuwa kuna uhitaji wa kuitikia” 

Wizara ya Maji Uganda yalinganisha madhara ya sasa na ya 1962

Wizara ya Maji na Mazingira nchini Uganda inasema madhara ya mafuriko kipindi hiki yamekuwa makubwa zaidi kutokana na kuharibiwa kwa maeneo oevu ikilinganishwa na 1962. 
 
Ilisajili kiwango cha juu zaidi cha maji mnamo Mei 2021 cha mita 13.50 tofauti na kiwango cha juu zaidi cha mita 13.41 katika mwaka 1964. 
 
Hata hivyo ilipofikia Januari 2022 kiwango cha maji kwenye Ziwa Victoria kilikuwa kimepungua hadi mita 11.76.  Ziwa Kyoga hadi 13.03 huku Ziwa Albert lililo chini kwenye mkondo wa Mto Nile nchini Uganda likiwa kwa mita 13.88. 

Viwango vya maji katika maziwa Albert, Victoria na Kyoga hadi mwezi Januari mwaka huu wa 2022
UN News
Viwango vya maji katika maziwa Albert, Victoria na Kyoga hadi mwezi Januari mwaka huu wa 2022

Beatrice Anywar ni Naibu Waziri wa Maji na Mazingira na anasema, “Tunahitaji kuendelea kuhamasisha watu wetu kukubali kwamba maeneo oevu huwa ni hifadhi za maji ya ziada yanapoteremka. Hutusaidia pia kudhibiti uchafu na kupunguza kasi ya maji hayo kwenye mkondo wake” 
 
Mafuriko yalionzia Ziwa Victoria yamehusishwa na mvua kubwa zilizonyesha nchini Rwanda, Kenya na Tanzania ambapo Bi. ANywar anasema, “Nataka nikwambie na Waganda wote wanaosikiliza kwamba tuna maji mengi zaidi katika Ziwa Victoria. Ni mengi zaidi kuliko tulivyowahi kushuhudia yanahatarisha bwawa letu la umeme. Ndio maana tuliamua kufungua maji haya ili yarejee kwenye kiwango kinachowezesha bwawa kuendelea. La sivyo tulikuwa katika hatari ya bwawa hilo kuvunjika ambalo lingekuwa janga kubwa la taifa” 
 
Kwa hiyo “na tunapofungua maji hayo kwa wingi, yanaateremka kwenye mkondo wake kwa wingi zaidi na ndio maana madhara makubwa zaidi yanaonekana kwenye Ziwa Kyoga na Ziwa Albert. Kwa uhakika wakaazi wanashuhudia mafuriko bila hata mvua. Wanajiuliza maji yanatoka wapi? Lakini li lazima tuyafungue ili kuokoa bwawa” 
 
Kutokana na mfano wa mafuriko miaka hii miwili, Uganda inaimarisha mfumo wa kupeana taarifa kuhusu tabianchi na nchi zinazoshiriki Mto Nile na zile za Ziwa Victoria na pia “Mpango wa kudumu tulionao kama serikali ni kujenga vifaa yya kuhifadhi maji ya ziada. Tayari tunachora miundo mbele ya ujenzi wa miundombinu ya kuhifadhi mkando aji na vyanzo asili vya maji vilivyofurika. Tunajua kwamba mvua inanyesha lakini haitanyesha milele. Msimu wa kiangaza utakuja na hifadhi hizo ndizo zitasaidia katika umwagiliaji” 
 
Wizara ya maji na mazingira inasema ilipofikia mwishoni  mwa Januari 2022 kiwango cha maji kilikuwa kinapungua kwa sentimita 1 kwa siku. 

Hata hivyo inatabiri kuwa kiwango cha maji kinaweza kupanda zaidi kufuatia mvua za mwezi Machi na April, na kuwaonya waliopoteza makaazi wasirejee kwa matumaini ya upungufu uliopo.