Niger yapongezwa kwa ukarimu kwa wasaka hifadhi na wakimbizi

10 Februari 2022

Viongozi wa mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa likiwemo lile la Kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi na lile la Uhamiaji IOM Antonio Vittorino wamefanya ziara nchini Niger, huko Agadez ambalo ni eneo la mpito la watu wanaotafuta hifadhi na wahamiaji nchini Niger ambalo limeongezeka kuwa na idadai kubwa ya watu wenye kuhitaji msaada wa usalama na fursa. 

Jamhuri ya Niger, taifa hili lisilo na bahari lililopo Magharibi mwa Afrika limepakana na mataifa saba ya ambayo ni Chad, Benin, Algeria, Nigeria, Mali, Burkina Faso na Libya. Kupakana na mataifa hayo kumeifanya nchi hii kuwa kitovu au njia ya wanaoelekea kaskazini mwa Libya, Algeria, na Bahari ya Mediterania.

Kwa sasa nchi hii inashuhudia kuongezeka kwa idadi ya watu wanaokimbia Libya au kufukuzwa kutoka Algeria. 

Mmoja wa watu hao ni Safa  Ahmed yeye alikimbia Sudan miaka mitano iliyopita na kukwama nchini Libya. Lakini sasa amefanikiwa kusafiri hadi hapa Agadez nchini Niger. “Kusema ukweli maisha ya hapa, mbali na kwamba sina mama na baba yangu ni mazuri. Asante Mungu. Ninafanya kazi, binti zangu wanasoma tena kwa Kiingereza. Nina biashara ya kuuza nguo na manukato. Naweza kufanya kazi. Sitarajii chochote kutoka kwa mtu yeyote. Nina kila kitu. Kwenye fikra zangu nimeshaachana na Libya.”

Kauli yake inaungwa mkono na Mkimbizi huku kutoka Cameroon ambaye anasema  “Tunamshukuru Mungu kwamba serikali ya Niger ilitupokea na kutupa mahali pa kulala na tunashukuru sana lakini sisi hapa, shida yetu kuu ni maisha yetu ya baadaye.”

Katika jiji la mbali la jangwa la Agadez, wanaotafuta hifadhi na wahamiaji wanaishi pamoja na wenyeji wao wananchi wa Niger.
© UNHCR/John Wendle
Katika jiji la mbali la jangwa la Agadez, wanaotafuta hifadhi na wahamiaji wanaishi pamoja na wenyeji wao wananchi wa Niger.

Ukarimu wa Niger unamfurahisha Filippo Grandi, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa anahusika na Wakimbizi ambaye anasema lengo kuu la UNHCR ni kuhakikisha wale wanaotafuta ulinzi wanapata usaidizi na wanapata hifadhi. 

“Nimefurahi sana, tumekuja hapa kujaribu kuona majukumu yetu ni nini na jinsi ambavyo kwa pamoja, tunaweza kusaidia watu hawa katika harakati zao, wakazi wa eneo hili na mamlaka ya nchi ambayo inabaki kuwa wakarimu sana na iko tayari kukaribisha kila mtu.”

Pamoja naye ni Antonio Vittorino, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM ambaye anasema "UNHCR na shirika letu (IOM) kama sehemu ya Umoja wa Mataifa, kufuatia uamuzi wa Katibu Mkuu, tuna jukumu la kushiriki zaidi kushughulikia mahitaji ya wasaka hifadhi.”

Wengi wa wasaka hifadhi wamepokelewa katika Kituo cha misaada ya Kibinadamu, eneo lililopo nje kidogo ya Agadez ambapo wanapata huduma za afya, shughuli za kiuchumi, maji, makazi na chakula yakiwa ni miongoni mwa mahitaji mengine ya kimsingi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter