Tumesikitishwa na kifo hiki cha mtoto– UNHCR/IOM/UNICEF/OHCHR
Tumesikitishwa na kifo hiki cha mtoto– UNHCR/IOM/UNICEF/OHCHR
Mashirika ya Umoja wa Mataifa likiwemo la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, la Uhamiaji, IOM, la kuhudumia watoto, UNICEF na Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, OHCHR, wamesikitishwa sana na taarifa za kifo cha mtoto mchanga kilichotokea Jumapili wakati wa walinzi wa mpaka wa pwani wa Trinidad walipokuwa wanakizuia chombo kilichowabeba wavenezuela waliojaribu kuvuka mpaka wa kusini mashariki mwa visiwa hivyo vilivyoko katika bahari ya Karibea.
Taarifa ya pamoja ya mashirika hayo iliyotolewa nchini Panama imeeleza kuwa walinzi wa mpaka wa Pwani walianza kukizuia chombo hicho kilichowabeba wavenezuela kilipoingia katika himaya ya Trinidad na Tobago baharini.
Kwa mujibu wa walinzi wa Pwani, mwanamke mmoja na mtoto mchanga walijeruhiwa katika tukio hilo. Mwanamke huyo alipelekwa katika kituo cha afya lakini kwa masikitiko makubwa mtoto alifariki dunia.
Mwakilishi Maalum wa UNHCR pamoja na IOM kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji wa Venezuela, Dkt. Eduardo Stein amesema, “tumesikitishwa sana na tukio hili la kusikitisha na tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia na wapendwa wanaoomboleza msiba huu na ahueni ya haraka kwa majeruhi. Hakuna mtu anayepaswa kupoteza maisha katika kutafuta usalama, ulinzi na fursa mpya. Tukio hili linaangazia masaibu wanayokumbana nayo watu wanaosafiri wakati wa safari za kutisha na hatari kuelekea kwenye usalama.”
Naye Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Amerika Kusini na Karibea, Jean Gough, ameongezea akisema, "hakuna mtoto mhamiaji anayepaswa kufa, iwe anasafiri na wazazi wake au peke yake. Hakuna mama anayetaka kuweka maisha ya watoto wake hatarini kwenye meli ndogo katika bahari kuu, isipokuwa hana chaguo lingine.Wavenezuela wawili kati ya watatu wanaohama ni wanawake na watoto.Tukio hili la kusikitisha ni ukumbusho tosha kwamba wao ndio walio hatarini zaidi miongoni mwa watu walio katika mazingira hatarishi.Wanastahili kuangaliwa, ulinzi na usalama wa pekee popote pale na wakati wowote.”
UNHCR, IOM, OHCHR na UNICEF wametoa wito kwa mataifa kuanzisha utaratibu utakaosaidia kulinda haki za watu wanaohama hasa wanawake, wasichana, wavulana na wengine wenye mahitaji maalum ya ulinzi ikiwa ni pamoja na haki ya kuhalalishwa kwa usahihi na taratibu za kupata hifadhi.