Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Machifu Sudan Kusini wajengewa uwezo ili wawalinde watoto

Watoto waliokimbia makazi yao nchini Sudan Kusini
© UNMISS / Eric Kanalstein
Watoto waliokimbia makazi yao nchini Sudan Kusini

Machifu Sudan Kusini wajengewa uwezo ili wawalinde watoto

Amani na Usalama

Katika kuhakikisha watoto wanaoishi kwenye maeneo ya mizozo ya kivita hawahusishwi kuingia vitani, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto UNICEF wamewakutanisha pamoja zaidi ya machifu 80 wa Sudan Kusini ili kuwapatia elimu ya kukomesha na kuzuia ukiukwaji wa haki za watoto.

Video ya Ujumbe wa kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS ikionesha ukumbi uliojaa viongozi wa kimila, wengi wao wakiwa wamevalia mavazi ya kaki na kofia zilizopambwa na kitambaa chenye mistari mwekundu na nyeupe, pamoja nao ni maafisa wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa serikali ya Sudan Kusini.

Kinachojiri  katika mkutano huo ni mafunzo na Naibu Mwakilishi wa UNMISS Sara Beysolow Nyanti anawaeleza viongozi hawa kuwa maendeleo ya nchi hii yanaanzia kwenye jumuiya ambazo wao ndio wanaziongoza.

"Ni katika ngazi ya jamii ambapo viongozi wa kimila wanaweza kuwa na jukumu kubwa la kudumisha amani kwa kuhakikisha kwamba katika ngazi ya jamii kunakuwa na amani ya watoto kwenda shule, amani ya watoto kukua, kustawi na kufikia malengo yao ya maendeleo. Wewe ni sehemu muhimu sana kwa watoto wa Sudan Kusini.“

Kauli hii ya inaungwa mkono na Daniel Achouth, Mkurugenzi Mtendaji, kutoka ofisi ya Makamu wa Rais, anayeshughulikia jinsia. “Wajibu wa machifu katika nchi hii ni muhimu zaidi. Na serikali ya Sudan Kusini inafahamu. Wakati wa mapambano ya ukombozi machifu wa Sudan Kusini walikuwa na jukumu kubwa la kuwahamasisha vijana kupigania uhuru wa Sudan Kusini, na ndiyo maana tuna Sudan Kusini leo. Kama tusingekuwa na nyinyi kama machifu, tusingekuwa na nchi inayoitwa Sudan Kusini. Kwa hiyo, kwenye suala la watoto na tunaamini uvunjifu wa haki za mtoto utakoma, kwa sababu kila jamii tuliyo nayo, tuna machifu na hakuna atakayefika huko na kufanya lolote bila taarifa yako.”

Naye Mawan Chol, Chifu Mkuu anakiri ushawishi wao ni mkubwa na wanaweza kusaidia kulinda watoto. "Sisi machifu tunaweza kulinda vijiji vyetu. Ikiwa kuna kiongozi yeyote wa kisiasa anayekuja kwetu na kusema kwamba anataka watoto wawafuate ili waende kupigana, sisi wakuu tuna haki ya kusema hapana, kwa sababu hatutaki watoto wetu wapigane. Tunachohitaji ni barabara, shule, maji safi na hospitali. Haya ndiyo tunayohitaji kuzungumza. Machifu hawana haki ya kuhamasisha watoto kwenda kupigana na jamii nyingine.”

Nalo shirika la UNICEF limesema linawatazamania viongozi hao wa kimila kuunga mkono mabadiliko na mageuzi na kuendeleza ulinzi wa walio hatarini zaidi hasa watoto, wanawake, wazee na walemavu.