Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kama si mimi kupambana na ukeketaji, nani mwingine? - Jaha Dukureh

Jaha Dukureh kwenye mjadala wa jopo kufuatia uzinduzi wa 'Ahadi ya Jaha', tukio lililoandaliwa na UN Women na Wallace Global Fund, lililofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani tarehe 6 Juni, 2017.
UN Women/Ryan Brown
Jaha Dukureh kwenye mjadala wa jopo kufuatia uzinduzi wa 'Ahadi ya Jaha', tukio lililoandaliwa na UN Women na Wallace Global Fund, lililofanyika katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani tarehe 6 Juni, 2017.

Kama si mimi kupambana na ukeketaji, nani mwingine? - Jaha Dukureh

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO linaeleza kuwa ukeketaji ni taratibu zote zinazohusisha kuondolewa kwa sehemu kiasi au sehemu yote ya nje ya uke wa mwanamke au kusababisha jeraha jingine katika viungo vya uzazi wa mwanamke kwa sababu zisizo za kimatibabu.

Ingawa kuna mjadala mpana kuhusu utamaduni huu uliopitwa na wakati ulianza lini, lakini utafiti wa vyanzo tofautitofauti unaonesha kuwa jambo hili limekuwepo kwa miaka mingi hadi pale ambapo limeonekana kuwa ni tatizo kubwa la kiafya na kijamii linalosalia katika maisha ya aliyekeketwa na mwishowe tatizo kubwa zaidi la pengo la usawa wa kijinsia. 

Soundcloud

 

Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau wake pamoja na wanaharakati wengine kote duniani wanafanya kila njia kutokomeza ukeketaji na hoja kuu ya sasa ni uwekezaji katika harakati za kutokomeza mila hiyo potofu inayotumbukiza takribani wasichana zaidi ya milioni 4 kila mwaka katika ukatili huo. 

Mwanaharakati mwenye asili ya Gambia Jaha Dukureh ni manusura wa ukeketaji na pia ndoa za utotoni za kulazimishwa. Akiwa Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake, UN Women Kanda ya Afrika, kwa kushirikiana na wanaharakati wengine duniani kote, amejitolea kukomesha ukeketaji kwa kuhamasisha vijana na kuongeza ufahamu wa mila hizi zenye madhara. Jaha anasema, “wasichana wana haki ya uhuru wa mwili wao na sio juu yetu sisi wanajamii kuamua ni nini kinachokatwa au kisichokatwa.” 

WHO inaeleza kuwa zaidi ya wanawake na wasichana milioni 200 walio hai katika nchi 30 wamekeketwa. Mmoja wao ni huyu Jaha ambaye anaeleza suala hili lilivyomtia katika matatizo makubwa akisema, “nilikuja kwenye jiji la New York Marekani Siku ya Krismasi nilipokuwa na umri wa miaka 15 ili kuolewa na mwanamume ambaye sikuwahi kukutana naye. Hapo ndipo nilipogundua kuwa nilipitia ukeketaji wa aina ya tatu ambayo ilimaanisha kuwa nisingeweza kufanya tendo la ndoa hadi nilipokatwa tena kufunguliwa njia.” 

Wale ambao wamekeketwa wanakabiliwa na hatari za kiafya kama vile maumivu makali, kutokwa na damu nyingi, mshtuko na maambukizi. Pia wanakabiliwa na hatari za muda mrefu kwa afya yao ya uzazi na akili. Jaha kwa kuwa aliyapitia haya na kwa kutambua kuwa kuna wengine wanaendelea kuyapitia, aliamua kupaza sauti.

"Nilianza kupaza sauti bila kujulikana wakati nilipokuwa na ujauzito wa binti yangu, nilijua kuwa sitaki binti yangu apitie hilo. Lakini pia nilijua kwamba kuna mamilioni ya wasichana huko nje ambao ni kama binti yangu, na hakuna mtu aliyekuwa akiwasemea. Na kama si mimi, ni nani mwingine?" Anaeleza Jaha Dukureh.

Jaha Dukureh, Balozi Mwema wa UN Women katika kutokomeza ukeketaji, FGM na ndoa za utotoni.
UN News/Dianne Penn
Jaha Dukureh, Balozi Mwema wa UN Women katika kutokomeza ukeketaji, FGM na ndoa za utotoni.

 

Ukeketaji umetapakaa katika maeneo kadha duniani na ndio maana mapambano dhidi yake yanahusisha dunia nzima. Ukeketaji wa anina ya tatu anaousema Jaha ni pale ambapo sehemu kubwa ya eneo la nje la uke inakatwa na wakati mwingine njia kuzibwa. Mwanamke mwingine ambaye anaeleza kufanyiwa hivyo ni Asil Ahmed wa Somalia.  

“Maumivu na uchungu wa kupata ukeketaji wa aina ya 3 na kupitia mchakato wa kukatwa na kushonwa ni kwa sababu ya kutojua. Hakuna msichana wangu atakayekeketwa na nitamshauri yeyote nitakayekutana naye dhidi ya mila hii. Nitawaambia wasikate na kuwashona binti zao.” 

Dkt. Maryam Omar Salad anayehudumu katika Hospitali ya Benadir, katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu anaonesha anaonesha anavyokerwa na ukeketaji akisema, "ukiua au kutoa sehemu yoyote ya mwili wa mtu yeyote, inachukuliwa kama uhalifu na nadhani serikali inaweza kuchukua jukumu kubwa katika kukomesha ukeketaji." 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kupitia ujumbe wake kuhusu suala hili la ukeketaji alioutoa katika siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji anasema ukeketaji ni ukiukaji wa kuchukiza wa haki za binadamu unaosababisha madhara makubwa na ya kudumu kwa wanawake na wasichana duniani kote. Umoja wa Mataifa na wadau wake wanaunga mkono mipango na miradi ya kubadili imani za kijamii zinazosongesha mila hiyo potofu.