Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahudumu wa afya wajengewa uwezo kukabili ukeketaji au FGM

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8 ambaye anaishi kwenye kituo cha kutunza watoto waliokimbia ndoa za lazima na ukeketaji, FGM
© UNICEF/Henry Bongyereirwe
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 8 ambaye anaishi kwenye kituo cha kutunza watoto waliokimbia ndoa za lazima na ukeketaji, FGM

Wahudumu wa afya wajengewa uwezo kukabili ukeketaji au FGM

Afya

Kuelekea siku ya kimataifa ya kutokomeza ukeketaji wa wanawake na wasichana, FGM, tarehe 6 mwezi huu wa Februari, shirika la Umoja wa Mataifa la afya  ulimwenguni, WHO hii leo limezindua mbinu mbili za kusaidia wahudumu wa afya kuwapatia tiba bora zaidi wanawake na wasichana waliokumbw ana ukatili huo, na halikadhalika kuunga mkono juhudu za kimataifa za kutokomeza FGM ambayo ni kitendo cha ukiukwaji wa haki za binadamu.
 

Mbinu hizo ni ile ya kuwezesha mawasiliano ya kibinafsi kati ya mhudumu wa afya na manusura na pili ni ile inayojumuisha  suala la FGM katika mtaala wa wakunga na wauguzi.

Mbinu hizi ni zaidi ya utabibu wa kovu

WHO inasema zaidi ya kutibu jeraha litokanalo na kukeketwa, wahudumu wa afya wana uwezo wa kusaidia madhila mbalimbali yanayotokana na FGM kwa wasichana na wanawake.

Mathalani madhara ya kimwili na kiakili na yale yanayoathiri afya ya kujamiiana. “Halikadhalika wana dhima m,uhimu ya ushawishi na hatimaye kubadili mtazamo wa watu kwa ukeketaji na hatimaye kuzuia matukio mapya ya ukeketaji.”

WHO inasema licha ya nafasi hiyo muhimu, bado wahudumu wa afya hadi sasa hawakuwa na mafunzo au msaada wanaohitaji kufanikisha jukumu hilo. “Na zaidi ya hayo hivi karibuni kumekuweko na kitendo cha ukeketaji unaofanywa na wauguzi, hali ambayo ni kama inakuwa inahalalisha kitendo hicho kiovu.”

Mwongozo huu mpya wa kuwezesha mawasiliano ya kibinafsi kati ya mhudumu wa afya na manusura unasaidia wahudumu wa afya kuchunguza maadili yao wenyewe kwa FGM na kujenga ufahamu na stadi zao ya jinsi ya kujengea uwezo wateja wao na kufikia uamuzi wa kukomesha kitendo hicho haramu.

Wahudumu wa afya wanajengewa uwezo wa mbinu ya mawasiliano bora kwa manusura na hivyo baada ya kupata mafunzo “washiriki wanaweza kujadili na wanawake juu ya imani zao kuhusu ukeketaji, na mashauriano hayo wanayafanya wakati wakiwa kliniki kabla ya kujifungua, na vile vile kusaidia kuhamasisha wanawake kufikiria upya kuhusu imani zao kwa ukeketaji.”

Mbinu zitawezesha wauguzi ,wakunga na wahudumu wa afya kusema HAPANA

Christina Pallitto, mwanasayansi wa WHO n mtaalamu kuhusu masuala ya FGM anasema, “msimamo wa WHO uko wazi: hakuna uhalalishaji wowote uwe kitabibu au vinginevyo- katika kukeketa mwanamke au msichana. Husababisha maumivu na madhara na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu. Hata hivyo itakuwa vigumu pindi wahudumu wa afya wanapoagizwa na mwanafamilia kufanya ukeketaji. Mafunzo haya mapya yatasaidia kuwezesha wahudumu wa afya kusema HAPANA na zaidi ya yote kusikiliza watu wanaowahudumua na kuwajengea uwezo wa kubadili mawazo yao kupitia mbinu inayojali mtu.”

Utafiti umeonesha kuwa mtaalamu wa kufundisha wauguzi na wakunga nao pia hauna taarifa sahihi za jinsi ya kuzuia ukeketaji na kuwahudumia wasichana na wanawake waliokeketwa, ambao hukumbwa na madhara makubwa ya kiafya. Na ndio maana mbinu ya pili imetolewa na imeshachapishwa kuziba pengo hilo.