Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusitishe mapigano kwa heshima na maadili ya Olimpiki- Guterres 

Mwanamichezo akijiandaa kwa ajili ya Olimpiki za majira ya baridi zinazoanza nchini China.
IOC/Thomas Lovelock
Mwanamichezo akijiandaa kwa ajili ya Olimpiki za majira ya baridi zinazoanza nchini China.

Tusitishe mapigano kwa heshima na maadili ya Olimpiki- Guterres 

Amani na Usalama

Mashindano ya michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi kali yakianza Ijumaa ya tarehe 4 mwezi huu wa Februari mwaka 2022 huko nchini China, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametaka kila mtu kuzingatia azimio la sitisho la mapigano wakati wa mashindano hayo.

Wanamichezo wa kiwango cha juu wakiwa tayari huko jijini Beijing China na viunga vingine ya taifa hilo la bara la Asia kwa ajili ya mashindano hayo ya olimpiki ya majira ya baridi kali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anakumbushia makubaliano yaliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Desemba mwaka jana ya kusitisha mapigano. 

Katika ujumbe wake Guterres anasema wanamichezo wanashiriki mashindano hayo kwa misingi ya maelewano, kujituma na bila kuoneana. 

“Misingi hii inatuvutia sote. Azimio la Olimpiki kuhusu sitisho la mapigano linatoa wito kwa pande zote kusitisha mapigano katika kipindi chote cha mashindano ya olimpiki.” Amesema Guterres. 

Kwa mujibu wa azimio hilo, nchi zinatakiwa kusiweko na mapigano siku 7 kabla ya kuanza kwa michezo hiyo hadi siku saba baada ya kumalizika kwa mashindano ya olimpiki ya majira ya baridi kwa watu wenye ulemavu, ambayo yatafikia ukomo tarehe 13  mwezi ujao wa Machi. 

Katibu Mkuu amesema mapigano yakisambaa na mivutano ikiongezeka, ombi la sitisho la mapigano linatoa fursa ya kuamliza tofauti na kusaka njia bora ya amani ya kudumu. 

“Tunavyohaha kutokomeza janga la COVID-19, hebu na tuungane kwa mustakabali salama zaidi, wenye ustawi na endelevu kwa kila mtu. Natoa wito kwa kila mtu kuzingatia mkataba wa Olimpiki wa sitisho la mapigano wakati wa mashindano ya olimpiki sambamba na yale ya walemavu. Kupitia nguvu ya michezo, na maadili ya Olimpiki, hebu na tujenge utamaduni wa amani.” Ametamatisha Guterres. 

Azimio hilo lililopatiwa jina Kujenga dunia yenye amani na bora zaidi kupitia michezo na maadili ya Olimpiki, lilipitishwa kwa kauli moja na lilikuwa limewasilishwa na mataifa 173.