Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utupaji sigara hovyo unaathiri binadamu na viumbe wa baharini:UNEP

Vishungi vya sigara na ganda la plastiki kwa ajili ya kuvutia sigara vikiwa vimepatikana  wakati wa kusafisha ufukwe nchini Marekani
Unsplash/Brian Yurasits
Vishungi vya sigara na ganda la plastiki kwa ajili ya kuvutia sigara vikiwa vimepatikana wakati wa kusafisha ufukwe nchini Marekani

Utupaji sigara hovyo unaathiri binadamu na viumbe wa baharini:UNEP

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP limezindua kampeni ya kujenga uelewa na kuchukua hatua za kutunza mazingira na afya za wananchi kutokana na vipande vidogo vidogo vya plastiki katika machujio ya sigara.

UNEP inashirikiana na Sekretarieti ya Mkataba wa Mfumo wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani juu ya Udhibiti wa Tumbaku (WHO FCTC) katika kampeni hiyo itakayofanyika mtandaoni na inayohusisha kutumia watu maarufu na Vijana wachechemuzi wa masuala ya mazingira mitandaoni na mabalozi wa hiyari wa UNEP.

Ushirikiano huo unawezeshwa kupitia kampeni ya UNEP ya “Bahari Safi, muungano wa kimataifa unaojumuisha nchi 63 zinazojitolea kukomesha uchafuzi wa plastiki baharini.

Atif Butt, Mkuu wa Uhamasishaji wa Umma wa UNEP amesema, “Sekretarieti ya WHO FCTC ina utaalamu wa kiufundi wa athari za bidhaa za tumbaku sio tu kwa afya ya binadamu bali pia kwa mazingira, kwa kujiunga nasi  katika uanzishaji wa Bahari Safi bila vipande vya plastiki, tunalenga kuangazia jinsi afya yetu inavyohusishwa na ile ya sayari yetu."

Kampeni hiyo pia Pia itatumia mwelekeo wa ushawishi wa kisiasa, ikitumia utaalamu wa WHO FCTC.

Kwakutumia maelekezo ya hivi karibuni ya Muungano wa Ulaya yanayotaka bdihaa zote za tumbaku zilizo na vichungi vya plastiki kuwekewa lebo inayoeleza wazi, kampeni hiyo itahimiza wananchi kupigia chepuo mabadiliko kama hayo duniani kote.

Naye Mkuu wa Sekretarieti ya WHO FCTC Adriana Blanco Marquizo amesema, “Sekretarieti ya WHO FCTC inafuraha kushiriki katika Kampeni ya Bahari Safi ya UNEP na imejitolea kusaidia kuongeza uelewa kuhusu suala la plastiki iliyofichwa kwenye sigara. Nawaomba nyote kujiunga na kampeni hii. Hebu sote tufanye sehemu yetu kuhakikisha bahari yetu pamoja na wakazi wake wote  wanalindwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

Bahari Safi na Sekretarieti ya WHO FCTC wamejitolea kuleta mabadiliko ya maana kwenye plastiki ndogo kwa kuongeza uhamasishaji na mabadiliko ya kisera. Ushirikiano huu unaashiria hatua muhimu ya kwanza kuelekea kupata  kusuluhisha la athari za kiafya na kimazingira za plastiki ndogo kwenye vichungi vya sigara.

Plastiki ndani ya sigara

Kila mwaka, tasnia ya tumbaku huzalisha sigara trilioni sita zinazotumiwa na wavutaji sigara bilioni moja duniani kote. Sigara hizi zina vichujio vinavyojumuisha hasa plastiki ndogo zinazojulikana kama nyuzi za acetate za selulosi. Sigara zinayotupwa hovyo vitako yake ( Vichungi)  huvunjika kutokana na sababu mbalimbali kama mwanga wa jua na unyevunyevu na hapo ndio hutoa plastiki ndogo pamoja na kemikali nyingine nyingi, hivyo kuathiri afya na huduma za mifumo ikolojia.

Kitacho cha sigara ndicho takataka inayotupwa zaidi duniani kote, ikichukua takriban kilo milioni 766.6 za takataka zenye sumu kila mwaka. Pia takataka hii ya plastiki ni kawaida kutupwa kwenye fukwe za bahari na kufanya mifumo ya ikolojia ya baharini kuathiriwa zaidi na uvujaji wa kemikali kuingia baharinina kusababisha vifo vya muda mrefu katika viumbe vya baharini, ikiwa ni pamoja na ndege, samaki, mamalia, mimea na wanyama watambaao.

Kemikali hizo huingia kwenye mzunguko wa chakula na huusishwa na madhara makubwa ya afya ya binadamu, ambayo yanaweza kujumuisha mabadiliko ya jenetiki, maendeleo ya ubongo, viwango vya kupumua na mambo mengine zaidi.