Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maambukizi mapya ya VVU mwaka 2020 miongoni mwa watoto yangezuilika - UNAIDS

Bango likikumbusha watu kuzuia UKIMWI na kuzitimiza ahadi zao za kufanya hivyo. UNICEF inasaidia kukuza uelewa kuhusu VVU na UKIMWI nchini Myanmar.
© UNICEF/Zar Mon
Bango likikumbusha watu kuzuia UKIMWI na kuzitimiza ahadi zao za kufanya hivyo. UNICEF inasaidia kukuza uelewa kuhusu VVU na UKIMWI nchini Myanmar.

Maambukizi mapya ya VVU mwaka 2020 miongoni mwa watoto yangezuilika - UNAIDS

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na UKIMWI, UNAIDS limeeleza kuwa katika maambukizi mengi mapya 150,000 ya Virusi Vya UKIMWI miongoni mwa wa watoto katika mwaka 2020, yangeweza kuzuiwa.

UNAIDS inasema maambukizi ya watoto 65,000 yalitokea mwaka wa 2020 kwa sababu wanawake ambao tayari wanaishi na VVU hawakutambuliwa wakati wa ujauzito na hawakuanza matibabu. Zaidi ya maambukizi 35,000 ya ziada ya watoto yalitokea kwa sababu wanawake walipata VVU wakati wa ujauzito au kunyonyesha, ambayo ilisababisha kuongezeka kwa kiwango cha virusi vyao na hatari kubwa ya maambukizi.  Zaidi ya maambukizi ya ziada ya watoto 38,000, inaeleza UNAIDS“yalitokea wakati akina mama walioanza matibabu ya kurefusha maisha hawakuendelea na matibabu wakati wa ujauzito na wakati wa kunyonyesha, na takribani maambukizi 14,000 yalitokea kati ya wanawake ambao walikuwa kwenye matibabu lakini virusi havikuwa vimefubazwa ipasavyo. Kuboresha ubora wa matibabu na matunzo ikiwa ni pamoja na utumiaji wa tiba bora zaidi na juhudi za kudumisha usaidizi wa marafiki (kama vile akina mama washauri) kunaweza kusaidia kuziba mapengo haya.” 

Aidha UNAIDS imesema wanawake walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU wanahitaji dawa maalum za kuzuia VVU, ikiwa ni pamoja na kuzuia PEP yaani dawa baada tu ya kuwa katika mazingira ambayo yanahisiwa kuwa yamesababisha maambukizi, ushauri wa kina zaidi, kurudia kupima VVU na utoaji wa vifaa vya kujipima kwa wenzi.