Afrika na ITU watambulisha masafa mapya ya redio
Afrika na ITU watambulisha masafa mapya ya redio
Wataalamu wa kimataifa wa mawasiliano ya redio kwa kushirikiana na nchi za Afrika hii leo wametambulisha masafa mapya kati ya 87.5 megahertz (MHz) na 108 MHz ili kupanua huduma za utangazaji za redio za FM ikiwa ni urekebishaji wa masafa katika bara zima.
Masafa mapya yaliyoratibiwa ni matokeo ya mradi wa miaka miwili wa uboreshaji wa Mpango wa GE84 kwa Afrika, unaoratibiwa kwa pamoja na Muungano wa Kimataifa wa Mawasiliano -ITU na Muungano wa Mawasiliano wa Afrika - ATU, kwa usaidizi shirikishi kutoka nchi 50 za Afrika.
Katibu Mkuu wa ITU Houlin Zhao akiwa Geneva Uswisi amesema kukamilika kwa mafanikio kwa mradi huu ni hatua kubwa kwa utangazaji wa redio barani Afrika, “upatikanaji wa habari kupitia teknolojia kama vile utangazaji wa redio ni muhimu ili kufikia Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. ITU inajivunia ushirikiano huu wenye manufaa na Umoja wa Mawasiliano wa Afrika ambao utaimarisha ufikiaji wa redio kote Barani Afrika.”
Naye Katibu Mkuu wa ATU John Omo alisema, “tunafuraha kwamba matokeo ya mradi huu yanafungua uwezekano kwa njia mpya kusaidia uendelevu wa muda mrefu wa utangazaji wa redio barani Afrika.”
Katibu Mkuu Omo aliongeza kuwa, “redio bado inatawala kama mfalme wa tasnia ya habari barani Afrika. Matokeo ya mradi huu yatachangia katika kujenga thamani kubwa ya kijamii na kiuchumi barani Afrika na kwingineko.”
Makubaliano ya masafa mapya
Kabla ya kufikia makubaliano ya kuwa na masafa mapya kulikuwa kunafanyika vikao mbalimbali kwa njia ya mtandano na kikao cha mwisho kilikusanya washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 45 za Afrika, pamoja na nchi 11 zinazopakana na Afrika.
Mario Maniewicz, Mkurugenzi wa Ofisi ya Mawasiliano ya Redio ya ITU amesema Utangazaji wa redio bado ni njia ya bei nafuu zaidi, ya kuaminika na inayoweza kufikiwa ya kusambaza habari barani Afrika na kwamba, “nchi lazima sasa zifanye vyema juu ya kujitolea kwao kugawa masafa zaidi kwa utangazaji wa FM. Watu katika bara ( la Afrika) wanahitaji ufikiaji wa zana hii muhimu ya mawasiliano,”
Manierwicz pia amezisihi serikali za Afrika, wadhibiti wa mawasiliano na watoa huduma kutumia kikamilifu njia hizo mpya zilizotambuliwa.
Kuhusu mradi wa kuboresha masafa
Mradi wa Uboreshaji wa Masafa GE84 unahusu matumizi ya megahertz 87.5–108 MHz kwa utangazaji wa sauti ya FM katika bara la Afrika ulianzishwa katika Makubaliano ya Kikanda, Geneva Uswisi mwaka 1984.
Mpango huo ulizinduliwa nchini Afrika Kusini, Julai 2019, ukilenga kuhakikisha upatanifu kati ya kazi zilizopo na mpya za masafa ya utangazaji katika bendi ya 87.5–108 MHz na kuwezesha kuanzishwa kwa utangazaji wa sauti dijitali barani Afrika.
Mradi pia ulifanya uchambuzi wa uoanifu wa FM wa kikanda, kwa kutumia zana za programu zilizotengenezwa na Ofisi ya Mawasiliano ya Redio ya ITU kama msingi wa majadiliano na uratibu zaidi kati ya tawala za kitaifa na kikanda.
Mradi huo uliwaleta pamoja watangazaji wa kitaifa na wadhibiti kutoka kote barani Afrika na kanda jirani ili kuzingatia vipengele mbalimbali vya uratibu wa masafa, ikiwa ni pamoja na hatua ambazo nchi zinaweza kuchukua ili kuepuka kuingiliwa kwa madhara huku huduma za FM zikipanuka.