Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Komesha sheria za ubaguzi wa ukoma bila kuchelewa :UN

Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.
ILO/Fiorente A.
Mfanyabiashara aliyeathiriwa na ukoma akisubiri wateja mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Komesha sheria za ubaguzi wa ukoma bila kuchelewa :UN

Afya

Leo ni siku ya Ukoma duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka 2022 ni Umoja kwa Utu.

Mtaalam huru wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza ukoma na ubaguzi dhidi ya watu walioathiriwa na ukoma na wanafamilia wao Alixe Cruz amesema duniani kuna zaidi ya sheria 100 ambazo zinabagua watu walioathirika na ukoma na kuhimiza kuwa zinapaswa kukomeshwa. 

Curuz katika taarifa yake aliyoitoa ijumaa 21 Januari 2022 amesema  ni "aibu" kwamba serikali zinaendelea kutunga sheria dhidi ya wale wanaougua moja ya magonjwa ya zamani zaidi yanayojulikana kwa wanadamu.

“Umefika wakati kwa mataifa yote yanayohusika kufanya maamuzi ama kuendelea kuwa nazo sheria kama hizo za kibaguzi dhidi ya watu walioathiriwa na ukoma kwa kukiuka Sheria za Kimataifa za haki za binadamu, au kuondoa ubaguzi huo katika sheria bila kuchelewa”, alisema Mtaalamu Cruz.

Kuhusu siku ya Ukoma

Siku hii ya Ukoma huadhimishwa kila Jumapili ya mwisho ya Januari na ndio maana kwa mwaka 2022 inaandhimishwa Januari 30.

Dhumuni la siku hii ni kutoa fursa ya kusherehekea watu ambao wamekumbwa na ukoma, kuongeza ufahamu wa ugonjwa huo, na kutoa wito wa kukomesha unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na ukoma.

Kampeni yenye kauli mbiu ya "Umoja kwa Utu" inahimiza kuwepo na umoja katika kuheshimu utu wa watu ambao wamekumbwa na ukoma. Kampeni hii pia inaheshimu uzoefu wa maisha wa watu ambao wamepata ukoma kwa kuwapa fursa ya kutoa simulizi zao zilizowawezesha pamoja na kutetea ustawi wa afya ya akili na haki ya maisha yenye heshima bila unyanyapaa unaohusiana na magonjwa.

Ujumbe muhimu 

1.    Kwa pamoja tunaweza kuinua kila sauti na kuheshimu uzoefu wa watu ambao wamepitia ukoma.
2.    Watu walio na ukoma wanakabiliwa na changamoto za ustawi wa afya ya akili kutokana na unyanyapaa, ubaguzi, na kutengwa.
3.    Watu walio na ukoma wana haki ya maisha yenye heshima bila unyanyapaa na ubaguzi unaohusiana na magonjwa.