Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yatumia wanajamii kuhamasisha utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 Goma, DRC

Muuguzi Jeanne Dusungu akimpa mgonjwa chanjo ya COVID-19 katika Hospitali ya Mkoa huko Goma, DR Congo, kama sehemu ya kampeni ya chanjo inayoongozwa na UNICEF.
© UNICEF/ Olivia Acland Kampeni ya chanjo dhidi ya Covid-19 nchini DR Congo

UNICEF yatumia wanajamii kuhamasisha utoaji wa chanjo dhidi ya COVID-19 Goma, DRC

Afya

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC shaka na shuku kuhusu chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19 zimekuwa chanzo cha kusuasua kwa kazi ya utoaji wa chanjo katika taifa hilo la Maziwa Makuu lakini harakati za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF za kuhamasisha wanachi zinaendelea kuzaa matunda na hata wale waliokuwa wanapinga sasa wanakubali kupatiwa chanjo.

Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Riziki Luanda, mkazi wa kitongoji cha Katindo anaongelea shaka na shuku kuhusu chanjo dhidi ya coronavirus">COVID-19, mazingira ambayo yameenezwa na taarifa potofu kuhusu chanjo hiyo. 

Mkazi mwingine wa hapa Katindo, Chibalonza Ikungu anafunguka zaidi, “baadhi ya watu  wanasema kuwa hii chanjo imeletwa kuchomwa kwa miili ya watu. Kama hatujachanjwa hatuwezi kwenda sokoni kununua vitu, huwezi kuingia kanisani au kuvuka mpaka. Hata hivyo sifahamu kama hii ni ukweli au la.” 

Mazingira haya yamesababisha shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kuingilia kati na kutumia wafanyakazi wa kujitolea kuendesha kampeni za kuongeza uelewa na kuondoa mtazamo hasi dhidi ya chanjo ya Corona. 

Miongoni mwa wafanyakazi hao ni Deogratius Mulahuko, Rais wa Kituo cha Afya cha Jamii mjini Goma ambaye anasema, “kwanza kabisa sisi ni daraja kati ya mamlaka na jamii. Ndio maana tunaitwa wapasha habari. Hawa ni kaka zetu, shangazi zetu. Mkakati wetu unahakikisha kuwa jamii inaelewa. Na kwa kufanya kazi kwenye jamii, jamii inatufahamu.” 

Deogratius anafanya kampeni ya mguu kwa mguu, mtaa kwa mtaa huku mfanyakazi wa kujitolea Bulonza Rutangira Noella akifunguka anasema,“nimekuwa afisa kiungo wa jamii hapa jimboni Kivu Kaskazini kwa miaka miwili sasa. Jirani yangu alikuwa akifanya kazi hii, amefariki Dunia. Lakini kwa sababu ya mazuri yote aliyotufanyia, niliamua kufanya kazi hiyo pia.” 

Deogratius anarejea tena na kusema, “kila ijumaa, tunafanya kampeni ya uhamasishaji kuhusu COVID-19, hasa kuonesha jamii kuwa ugonjwa bado uko, haujaisha. Tumepata changamoto nyingi na ugonjwa huu, lakini tutaendelea kuhamasisha kwa sababu tunaelewa kwamba uhamasishaji ni mchakato na mabadiliko hayatokei mara moja.” 

Na sasa walioelewa kama Dieumerci Matabaro mkazi wa Katindo wanasema, “Corona iko, kila mtu apatiwe chanjo kwa sababu ni ugonjwa unaosambaa duniani kote. Natarajia kuwa wa kwanza kupatiwa chanjo ili kuwa mfano kwa sababu mimi ni kijana namba moja hapa.”