Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuchukue hatua kupinga chuki dhidi ya wayahudi na nyinginezo- Guterres 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres  akihutubia kwenye sinagogi la Park East jijini New York, Marekani (31 Oktoba 2018)
UN /Rick Bajornas
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia kwenye sinagogi la Park East jijini New York, Marekani (31 Oktoba 2018)

Tuchukue hatua kupinga chuki dhidi ya wayahudi na nyinginezo- Guterres 

Haki za binadamu

Kila mtu, kokote pale aliko lazima asimame kidete dhidi ya chuki, wakati huu wa ongezeko wa chuki dhidi ya wayahudi na aina nyingine za ubaguzi wa kidini,  amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo jijini New York, Marekani. 

Wito wake huo ameutoa kwa njia ya video katika ibada iliyofanyika kwenye Sinagogi la Park East jijini New York, Marekani hii leo kuadhimisha miaka 77 tangu kukombolewa kwa kambi ya maangamizi ya Auschwitz. 

Ibada hiyo ya kila mwaka inalenga kukumbuka wayahudi milioni 6 waliouawa katika maangamizi yaliyofanywa na manazi wa kijerumani, na mwaka huu pia ibada hiyo imefanyika kwa njia ya mtandao kutokana na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19

Idadi ya manusura inapungua 

“Miaka 77 iliyopita, ukombozi ulitokomeza mauaji ya maangamizi. Lakini ilikuwa ni mwanzo wa juhudi zetu za kuhakikisha uhalifu kama huo katu hautatokea tena,” amesema Katibu Mkuu. 

“Kadri idadi ya watu wachache ndio wanaweza kutoa ushuhuda, hebu na tuahidi kukumbuka na kufanya jitihada ili tusisahau.” 

Bwana Guterres amerejelea hasara ya maangamizi hayo makubwa. Utawala wa manazi uliotowesha jamii nzima, na kuharibu kumbukizi ya kipekee ya maisha ya wayahudi barani Ulaya. 

Kiongozi wa sinagogi hilo, Rabi Athur Schneier ambaye alizaliwa huko Vienna, alinusurika mauaji ya maangaizi lakini baadhi ya wanafamilia wake waliuawa huko Auschwitz.  

“Kwa kunusurika, naahidi kuwa nitajitolea maisha yangu yote kusaidia kutokomeza chuki dhidi ya wayahudi na aina yoyote ya chuki ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu mwingine atapitia machungu ambayo yalielekezwa kwa wayahudi.” 

Chuki dhidi ya wayahudi inaibuka 

Katibu Mkuu ameelezea chuki dhidi ya wayahudi na aina nyingine za ubaguzi wa kidini vinachipukia kwa sababu kadri vinavyoenea na kuvuruga dunia, ndivyo kadri zinaweka nyufa kwenye misingi ya ubinadamu. 

Hii leo ni vigumu kupuuza nyufa hizi. 

“Chuki dhidi ya wayahudi- aina ya zamani zaidi ya chuki na ubaguzi inarejea tena. Karibu kila siku kuna ripoti mpya za mashambulizi kwa njia ya maneno au vitendo; makaburi au masinagogi yanaporwa au kufanyiwa uhalifu.” 

Katibu Mkuu amesema sambamba na hilo kupotosha au kukataa ukweli kuhusu mauaji ya maangamizi nako kunaongezeka. Amesema, “Jawabu letu kwa upotoshaji huu ni elimu. Serikali kila pahali zina wajibu wa kuelimisha kuhusu vitisho vya mauaji ya maangamizi.”