Skip to main content

Wanawake wengi sana wanaendelea kufa kutokana na utoaji mimba usio salama: WHO

Kuwalinda wanawake na wasichana kupitia utoaji mimba salama
Picha na WHO
Kuwalinda wanawake na wasichana kupitia utoaji mimba salama

Wanawake wengi sana wanaendelea kufa kutokana na utoaji mimba usio salama: WHO

Afya

Wasichana na wanawake wengi sana wanaendelea kufa na kukabiliwa na matokeo mabaya ya uavyaji mimba usio salama, hata hivyo kuna ukosefu wa taarifa kuhusu jinsi huduma bora inaweza kutolewa kwa wasichana na wanawake wenye matatizo yanayohusiana na utoaji mimba, limesema Shirika la Afya Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa, WHO.

WHO na wadau wake wamefanya utafiti katika nchi 17 za Amerika ya Kusini na Karibea. WHO imeshirikiana na HRP yaani Human Reproduction Program ambacho ni chombo kikuu cha mfumo wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya utafiti katika uzazi wa binadamu ili kuboresha afya ya uzazi. 

Nyongeza maalum ilitolewa hii leo Jumatano ambayo inaangazia kazi ya utafiti huu katika nchi 11 za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na katika Jarida la Kimataifa la Gynecology and Obstetrics (IJGO), inajumuisha nakala saba za utafiti na tahariri. 

"Utafiti  huu unaonesha safari tuliyonayo ili kuhakikisha huduma ya heshima na bora kwa wote baada ya kuavya mimba; pia inaonesha ni kiasi gani tunaweza kujifunza tunapojitolea kufanya kazi pamoja.” amesema Özge Tunçalp, Mshauri wa tiba wa WHO na HRP. 

Taarifa zilizokusanywa kwa wanawake 23,000 

Taarifa zilikusanywa kuhusu zaidi ya wanawake 23,000 wanaohudhuria vituo vya afya wenye matatizo yanayohusiana na uavyaji mimba katika nchi zilizofanyiwa utafiti. 

Taarifa ya WHO imeeleza kuwa, “ingawa wengi wa wanawake hawa walikuwa na matatizo madogo au ya wastani yanayohusiana na utoaji mimba, bado kulikuwa na wengi ambao walikuwa na matatizo makubwa au ya kutishia maisha, hasa katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.” 

Kutokana hali hiyo, nchi zimeshauriwa kuwa ni lazima zichukue hatua haraka ili kuhakikisha kuwa watoa huduma za afya na mifumo inaweza kutoa huduma bora kwa wasichana na wanawake. 

Nchi ziongeze ufikiaji wa huduma bora za utoaji mimba katika ngazi zote huduma ya afya na kuhakikisha mbinu za kuboresha ubora wa huduma baada ya kuavya mimba zinatokana na ushahidi ili kuhakikisha kwamba: watoa huduma za afya wanatumia mbinu zinazopendekezwa; kukagua upatikanaji wa vifaa; na kufanya ukaguzi wa kimatibabu ili kuelewa vyema sababu za matatizo ya kiafya au matokeo mabaya.