Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres atoa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi katika maeneo ya mijini 

Watoto wakiangalia gari lililoungua baada ya mashambulizi ya anga katika ukanda wa Gaza (Maktaba)
© UNRWA/Mohamed Hinnawi
Watoto wakiangalia gari lililoungua baada ya mashambulizi ya anga katika ukanda wa Gaza (Maktaba)

Guterres atoa wito wa kukomeshwa kwa mashambulizi katika maeneo ya mijini 

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres hii leo kupitia ujumbe wake kwa mjadala wa wazi wa Baraza la Usalama uliofanyika jijini New York, Marekani, amewahimiza nchi zote wanachama kutumia ushawishi wao kwa wadau na washirika wao kuhakikisha wanaheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu na kutenda matendo mema. 

Majadala huu wa wazi wa Baraza la Umoja wa Mataifa ulikuwa unajadili Vita katika miji: Kuwalinda raia katika mazingira ya miji.  

Aidha Katibu Mkuu Guterres amelieleza Baraza la Usalama kwamba lina jukumu muhimu katika suala hili akisema, “nategemea wajumbe wote wa Baraza kukiri changamoto za vita vya mijini, kuomba hatua mahususi za ulinzi, na kutumia zana zote walizonazo kukomesha madhara mabaya na yanayoweza kuzuilika kwa raia.” 

Bwana Guterres ameeleza kuwa katika nyakati za sasa, zaidi ya watu milioni 50 wameathiriwa na migogoro katika maeneo ya miji na wanakabiliwa na hatari kadhaa.  

"Uhasama unapotokea katika miji, raia wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi ya kuuawa au kujeruhiwa. Katika baadhi ya matukio, wanaweza kimakosa kudhaniwa kuwa wapiganaji. Katika maeneo mengine, madhara yatakayotokea kwa raia mara nyingi yanaonekana kabisa kabla, lakini pande zinazozozana hazichukui hatua za kuziepuka na kuzipunguza.” Ameeleza Katibu Mkuu Guterres.  

Bwana Guterres ameendelea kueleza kuwa wakati silaha za milipuko zinatumiwa katika maeneo yenye watu wengi, karibu asilimia 90 ya wanaouawa na kujeruhiwa ni raia. Raia wanaweza kupata madhara makubwa katika matokeo ya haraka, na kwa muda mrefu. Waathirika wengi wanakabiliwa na ulemavu wa maisha na majeraha makubwa ya kisaikolojia. Miundombinu ya maji, umeme na usafi wa mazingira mara nyingi huharibiwa. Huduma za afya zinatatizika sana. 

Kwa kutaja baadhi ya mifano, Bwana Guterres amesema, Shule nyingi na vituo vya afya viliharibiwa wakati wa mapigano huko Gaza mwaka jana. Takriban watu 800,000 waliachwa bila kupata maji ya bomba, hivyo basi kuongeza hatari ya magonjwa na kuzorotesha zaidi huduma za afya. 

Pia Guterres ameitaja Afghanistan akisema, “Shambulio la mlipuko nje ya shule ya sekondari ya Kabul mwezi Mei mwaka jana liliua wanafunzi 90, hasa wasichana, na kuwajeruhi wengine 240." 

Katika mifano mingine amezitaja Yemen, Libya, Syria na Yemen.