Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msimu wa baridi ni kama tunaishi katika jokofu- Mkimbizi wa Syria

Majira ya baridi kali yanaendelea kufanya maisha kuwa magumu kwa wakimbizi wa ndani katika kambi kama hii huko Idlib, Syria
Mark Cutts
Majira ya baridi kali yanaendelea kufanya maisha kuwa magumu kwa wakimbizi wa ndani katika kambi kama hii huko Idlib, Syria

Msimu wa baridi ni kama tunaishi katika jokofu- Mkimbizi wa Syria

Msaada wa Kibinadamu

Familia za wakimbizi wa ndani pamoja na zile zilizowakaribisha wakimbizi hao katika ukanda wa mashariki ya kati kwa sasa zinakabiliana na baridi kali kutokana na kuanguka kwa theluji wakati huu wanaishi kwenye mahema. 

Video ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR inaonesha madhila wanayokumbana nayo wakimbizi wa ndani wa Iraq, Syria, Jordan.

Katika maeneo mengi duniani makazi ya wakimbizi hujengwa kwa nyenzo ambazo nizamuda mfupi ndio maana vitu kama maturubai hutumika katika kujengea makazi ya muda ya wakimbizi. 

Lakini kila msimu huja na changamoto zake, wakimbizi wa ndani katika ukanda wa mashariki ya kati kwa sasa wapo katika msimu wa baridi na picha zilizopigwa kutoka angani zilionesha theluji imetanda na ardhini wakimbizi wa Syria wakijitahidi kuondoa theluji hiyo nje ya nyumba zao wanazoishi lakini baadae kidogo theluji inamwagika tena na kwenye mahema maisha ni magumu hasa wakati inamwagika usiku. 

Watoto wawili katika kambi ya Killi huko Idlib wakati wa miezi ya baridi kali huko Kaskazini Magharibi mwa Syria.
© UNOCHA
Watoto wawili katika kambi ya Killi huko Idlib wakati wa miezi ya baridi kali huko Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Wakimbizi walioko Kurdistan nchini Iraq nao wanapambana na maswahibu haya haya, kukipambazuka shughuli ni moja,  wanawake kwa wanaume wanakamata machepe na kupanda juu ya mahema kuondoa theluji na wengine wakiondoa ardhini. 

Picha iliyopigwa kutoka angani inaonesha kambi ya Zaatari iliyoko nchini Jordan ikionesha nyumba za wakimbizi zilizojengwa kwa mabati, wananchi wakitaka joto basi kuwasha moto nakupecha mikono.  Hali hii Khaled mkimbizi kutoka Syria anasema ni kama wanaishi kwenye friji. “Kambi ya Zaatari ni baridi sana; makazi yetu ni kama masanduku ya barafu,kama friji. Mara tu ninapozima hita, inakuwa friji. Je, kuna mateso zaidi ya haya?”

Mvulana mdogo akipulizia mikono yake ili kuwapa joto katika kambi ya Killi huko Idlib wakati wa miezi ya baridi kali huko Kaskazini Magharibi mwa Syria.
© UNOCHA
Mvulana mdogo akipulizia mikono yake ili kuwapa joto katika kambi ya Killi huko Idlib wakati wa miezi ya baridi kali huko Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Kambi zote hizi zipo chini ya uangalizi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ambao wanasema kuna baadhi ya wakimbizi huu ni msimu wa 11 mfululizo wa baridi tangu wafurushwe makwao na wamekuwa wakiteseka hii. 

Shirika hilo katika msimu huu hutoa mahitaji muhimu kama vile nguo za joto, malazi, blanketi za joto na malipo ya dharura ya msimu wa baridi ili kuhakikisha familia zinaweza kununua kile wanachohitaji zaidi.

Mpaka sasa kuna kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani wa Syria na Iraq milioni 10 na wakimbizi kutoka nchini Syria, Iraq, Lebanon, Jordan na Misri, na zaidi ya watu milioni 3.3 kati yao wanahitaji usaidizi waharaka wa kukabiliana na majira ya baridi kali.