Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yaongeza wanafunzi katika shule za Serikali Uganda

Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.
© UNICEF/Maria Wamala
Mukasa Herbert mwanafunzi katika Shule ya Nakivubo Settlement Nursery na Primary School nchini Uganda ananawa mikono siku ya kwanza ya kufungua tena shule, Januari 10, 2022.

COVID-19 yaongeza wanafunzi katika shule za Serikali Uganda

Utamaduni na Elimu

Nchini Uganda wiki moja baada ya shule kufunguliwa ikiwa ni takribani miaka miwili tangu janga la COVID-19 kusababisha kufungwa wanafunzi na walimu wanakumbana na changamoto kubwa ya idadi kubwa ya wanafunzi kutoka shule binafsi kuandikishwa katika shule za bure na hivyo kusababisha miundombinu kuhelemewa. 

Jijini Hoima mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa John Kibego ametembelea maeneo kadhaa na kuzungumza na wadau kutaka kupata picha halisi na mipango ya viongozi wa serikali katika kutatua changamoto zilizojitokeza. 

Wanafunzi na walimu

Wanafuzi kwenye shule ya msingi ya Hoima public iliyoko katikati mwa mji wa Hoima walionekana kuendelea na masomo darasani. Shule hiii ya serikali inatoa elimu bure kwa wote.

Anet Kabasomi ni mwanafunzi wa shule hii ambaye anasema “Tumeanza vyema katika darasa la sita. Idadi ya wanafunzi inaongezeka kila siku na tunawashukuru wazazi kwa kutupatia watoto lakini yote kwa yote tunahitaji walimu zaidi kutusaidia”

Mwalimu Anet Kabasomi wa darasa la sita ameeleza changamoto ya idadi kubwa wanafunzi waliojitokeza karibu miaka miwili baada ya shule kufungwa kama njia ya kudhibiti mlipuko wa COVID-19 ambayo haiendani na miundombinu na hata idadi ya walimu walioko. 

Lakini wanafunzi wanajivunia kurejea shuleni na kuanza kusomeshwa katika mazingira yoyote yale kama anavyothibitisha msichana Madrin Atugonza wa darasa la saba. “Nyumbani kuna TV lakini kusomea kwenye TV mafunzo zayaingii kichwani, hata ukisoma vitabu. Kwa hiyo Raisi alipoamua kufungua shule nilifurahi sana” amesema Madrin Atugonza 

Akikumbuka alivyokuwa akijaribu njia mbalimbali kuhakikisha anaendelea kusoma akiwa nyumbani Madrin Atugonza anaeleza kuwa “Wakati wa COVID-19 tulikwenda na kuishi vijijini akini sikuwa na raha kwani hatukuwa tunasoma. Watoto wengine walikuwa wakisomea kwenye mtandao wa intaneti lakini sisi wazazi wetu hawakuwa na pesa. Tulikuwa tu tukisoma vitabu lakini masomo ya nyumbani hayaendi vyema”
Mmiminiko wa wanafunzi usiotarajiwa katika shule za serikali umeathiri kazi ualimu.
Jackson Irumba naye ni mwalimu hapa ambaye anasema “Changamoto kubwa tangu tuanze kusomesha Jumatatu mpaka leo ni idadi klubwa ya wanafunzi. Ukiangalia katika darasa la saba, mwaka jana tulikuwa a wanafunzi 135 waliofanya mtihani ya PLE lakini sasa ni takribani 200”

Na kufafanua kuhusu changamoto hiyo akisema “Unavyongalia ufuatilia darasani, wanafunzi wamesongamana na pia kupita kati yao ni vigumu. Inamaanisha kwamba mwalimu kushughulikia mahitaji ya mtoto binafsi ni vigumu”

Harriet Karungi Basemera ni Mwalimu Mkuu wa shule hii anaomba msaada ili waweze kushughulikia changamoto hizi. “Tunaendelea kusajili watoto kwani hii ni shule ya serikali na ya elimu ya bure kwa hiyo hatuwezi kuwafukuza. Tunaomba serikali kuziba mapengo ya walimu yalioko kwani idadi yao ni kubwa mno. Mwalimu ana tahini vitabu zaidi ya 200. Tunaomba wakubwa wetu wafikirie kutupatia mahema kwani madarasa hayatoshi”

Mkuu wa Elimu Hoima

Mkuu wa elimu katika jiji la Hoima, Johnson Kusiima Baingana, Mkuu wa elimu katika jiji la Hoima na hivi ndivyo alivyosema “Tumeshuhudia mmiminiko wa wanafunzi kutoka shule binafsi kutoka shule binafsi kuja shule za elimu ya bure hii ni kutokana na athari za COVID-19 kwakuwa sasa wazazi hawawezi kukidhi gharama za ada ya shule na mahitaji mengine.”

Baingana amewaomba wadau wote kutekeleza wajibu wao kuhakikisha elimu inaendelea “Natoa wito kwa wazazi na wadau wengine kuhakikisha kuwa elimu inaendelea vyema, shule nyingine za bure nawasihi kujenga mahema ili watoto waweze kuendelea na masomo.”

Wengi wa nanafunzi waliojitokeza kwanza ni wale wanaotoka kwenye shule za kipekee lakini bado kuna wengine wengi waliokuwa katika shule za serikali ambao hawajasajiliwa. 

Miongoni mwa sababu ya cangamototo hizi ni shule za kipekee kupandisha ada za shule zikisema gharama ya maisha imepanda sana.

Kuhusu hatima ya wasichana waliopata mimba wakiwa likizoni, Bwana Baingana anasema “Wizara ya elimu imekuwa bayana kuhusu hili kwamba lazima waruhusiwe kurejea shuleni na hasa pale ikiwa mimba haijavuka miezi mitatu na miezi sita baada ya mama kujifungua huku mama akiendelea kumnyonyesha mtoto.”
Kufunguliwa kwa shule umekuwa ufuguo muhimu kwa karibu sekta zote za uchumi. Wasafirihsaji, wachuuzi na hata wakulima wana uhakika sasa kuwa soko lipo.