Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mifumo ya elimu imepitwa na wakati, sasa ni lazima tuirekebishe- Guterres

Watoto wakijifunza kupitia kompyuta ndogo au Tablet kwenye shule moja huko Yaoundé nchini Cameroon
© UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakijifunza kupitia kompyuta ndogo au Tablet kwenye shule moja huko Yaoundé nchini Cameroon

Mifumo ya elimu imepitwa na wakati, sasa ni lazima tuirekebishe- Guterres

Utamaduni na Elimu

Ikiwa leo ni siku ya elimu duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema janga la COVID-19 na changamoto nyingine zinazokabili Dunia hivi sasa zimedhihirisha umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo Katibu Mkuu amesema “dunia yetu inabadilika kwa kasi ya haraka mno, ubunifu katika teknolojia, mabadiliko yasiyo ya kawaida kwenye dunia ya ajira, dharura ya mabadiliko ya tabianchi na kuenea kwa ukosefu wa imani baina ya watu na taasisi.”

Na zaidi ya yote, mifumo ya kawaida ya elimu inahaha kutoa elimu, stadi na maadili ambayo ni lazima kuijenga ili kuweko na mustakabali bora, salama na unaojali mazingira kwa wote.

Ametolea mfano wa janga la COVID-19 akisema limetibua sekta ya elimu duniani kote.
Takribani wanafunzi bilioni 1.6 wa Vyuo Vikuu na shule masomo yao yalivurugika janga tu la Corona lilipoanza na hadi sasa bado halijaisha.

Hii leo, ufungaji wa shule unaendelea kuvuruga maisha ya zaidi ya wanafunzi milioni 31 na kuchochea janga la kujifunza duniani.

Guterres anaonya “tusipochukua hatua, idadi ya watoto wanaoacha shule katika nchi zinazoendelea na ambao hawajui kusoma na kuandika inaweza kuongezeka kutoka asilimia 53 hadi asilimia 70.”

Mwanafunzi wa kike akiandika kwa makini akiwa darasani huku amevalia barakoa yake ya kushoneshwa nyumbani. Hapa ni katika shule ya msingi ya Mchoka wilaya ya Salima nchini Malawi, tarehe 13 Novemba mwaka 2020.
© NICEF/UN0372089/
Mwanafunzi wa kike akiandika kwa makini akiwa darasani huku amevalia barakoa yake ya kushoneshwa nyumbani. Hapa ni katika shule ya msingi ya Mchoka wilaya ya Salima nchini Malawi, tarehe 13 Novemba mwaka 2020.

Elimu ni zaidi ya hoja ya usawa

Katibu Mkuu amesema kuwa sakata la elimu ni zaidi ya hoja ya kuipata na ukosefu wa usawa kwa kuwa “elimu ni bidhaa ya umma na ni jambo muhimu linalohitajika kufanikisha ajenda nzima ya 2030 kwa maendeleo endelevu. Jamii ya kimataifa haiwezi kukubali kutokuwa na uhakika katika utoaji wa elimu, tena bora na inayoendana na wakati.”

Amesema ni kwa kutambua hilo ndio maana ataitisha baadaye mwaka huu mkutano wa viongozi wa kurekebisha mfumo wa elimu. “Muda umefika kuchochea upya azma yetu ya pamoja kwa elimu. Hii ina maana kuwekeza katika mipango thabiti ya kusaidia wanafunzi kupata mafunzo ambayo walipoteza.”

Ina maana kuiweka elimu katika kitovu cha juhudi pana za kujikwamua, zinazolenga kurekebisha uchumi na jamii na kuchochea kasi ya maendeleo endelevu.

Wanafunzi wanatumia kompyuta mpakato zilizotolewa na UNICEF katika shuke ya sekondari kwenye eneo la Sana'a Yemen.
© UNICEF/Hani Alansi
Wanafunzi wanatumia kompyuta mpakato zilizotolewa na UNICEF katika shuke ya sekondari kwenye eneo la Sana'a Yemen.

Zaidi ya yote, “ina maana mshikamano wa kifedha na nchi zinazoendelea. Na ina maana kuanza mchakato wa kutafakari, kuchambua na kubaini jinsi mifumo ya kitaifa ya  elimu inaweza kubadilika na kurekebishwa kati ya sasa na mwaka 2030.”

Amefafanua kuwa mkutano wa viongozi wa kufanyia marekebisho ya elimu utakuwa ni wa mara ya kwanza kwa viongozi wa dunia, vijana na wadau wote wa elimu wanakutana pamoja na kuzingatia masuala hayo ya msingi.

Ametamatisha ujumbe wake akisema "katika siku hii ya kimataifa ya elimu, na tunavyojiandaa kwa mkutano huo baadaye mwaka huu, natoa wito kwa kila mtu kuungana kwa ajili ya elimu kama bidhaa ya umma na kama kipaumbele cha juu cha kisiasa kwa ajili ya kujikwamua hivi sasa na zaidi.”