Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 1.5 hawapati matibabu dhidi ya tatizo la uzito mdogo Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika - UNICEF

Mtoto mwenye utapiamlo mkali akiwa katika kilniki nchini Ethiopia
© UNICEF/Esiey Leul
Mtoto mwenye utapiamlo mkali akiwa katika kilniki nchini Ethiopia

Watoto milioni 1.5 hawapati matibabu dhidi ya tatizo la uzito mdogo Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika - UNICEF

Afya

Takribani watoto milioni 1.5 katika maeneo ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, hawapati matibabu ya kuokoa maisha kutokana na uzito mdogo ikilinganishwa na urefu wao, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeonya leo.  

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na UNICEF katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, imesema, idadi hiyo inawakilisha karibu nusu ya watoto wanaokadiriwa kufikia milioni 3.6 wanaohitaji msaada wa dharura, ambao hawafikiwi kwa wakati ili kuokoa maisha yao au kuwaepusha na uharibifu wa kudumu. 

Nchi zilizofanyiwa utafiti ni Angola, Ethiopia, Sudan Kusini, Madagascar, Somalia, Kenya, na Msumbiji. 

Licha ya hatua za taratibu katika  kutibu utapiamlo, ukosekanaji wa ufikiaji wa matibabu katika eneo hilo, athari za janga la COVID-19, pamoja na majanga ya hali ya hewa na migogoro inayoendelea, inaendelea kusukuma watoto na familia ukingoni. Kwa kuongezea, mapungufu ya mara kwa mara katika ufadhili yanasalia kuwa kikwazo kwa mwitikio wa kibinadamu wa UNICEF. 

"Hakuna kitu kinachoumiza zaidi kuliko kuona watoto wakiteseka kutokana na unyafuzi mkali wakati tunajua kuwa ungeweza kuzuiwa na kutibiwa. Shukrani kwa msaada wa wafadhili na washirika wetu, tumefikia baadhi ya matokeo bora na hadithi za mafanikio; lakini athari za COVID19, mabadiliko ya tabianchi na migogoro vinaleta dhoruba ambapo mahitaji yanapita haraka rasilimali, na wakati wa kuchukua hatua ni sasa." Amesema Mohamed M. Fall, Mkurugenzi wa UNICEF Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika. 

UNICEF inasema kwa sasa, familia katika eneo lote zinakabiliana na migogoro mingi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa viwango vya uhaba wa chakula, kuzorota kwa uchumi, milipuko ya magonjwa, mizunguko isiyo ya kawaida ya mafuriko na ukame, na migogoro. Mamilioni ya watu wanalazimika kupunguza wingi au ubora wa chakula wanachokula ili waendelee kuishi. Mara nyingi, familia hulazimika kufanya yote mawili. 

“Hili ni janga la lishe linalokuja ambalo linaweza na lazima liepukwe.” UNHCR imeonya na kuongeza kuwa kwa ufikiaji usiozuiliwa na ufadhili unaotabirika wa kufikia watoto wanaohitaji, UNICEF na washirika wanaweza kuokoa maisha ya karibu kila mtoto anayelazwa kutokana na uzito mdogo katika eneo hilo. Kinga inasalia kuwa njia bora zaidi ya kuhakikisha kwamba watoto wanaishi, kuepuka uharibifu wa kudumu wa kiakili na kimwili, na kukwepa mateso ya maisha yote yanayotokana na utapiamlo wa utotoni. 

Shirika hilo la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa linaeleza kuwa hali katika eneo hilo tajwa bado ni mbaya na usumbufu wowote wa operesheni ya kibinadamu ambazo tayari zimeelemewa, inaweza kuzidisha kile ambacho tayari ni janga la lishe ya muda mrefu. 

UNICEF inatafuta dola za Marekani milioni 255 ili kuongeza hatua zake za dharura kutatua tatizo la lishe katika nchi zilizopewa kipaumbele katika Mashariki na Kusini mwa Afrika mwaka 2022, na kusaidia watoto kwa huduma za lishe za kutosha na za kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na matibabu ya unyafuzi mkali.