Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza Kuu la UN lapitisha azimio la kupinga upotoshaji na ukataaji wa mauaji ya halaiki, Guterres apongeza

Jengo la Shoah la kumbukizi kuhusu mauaji ya halaiki ambako elimu inatolewa kuhusu mauaji hayo.
UNESCO
Jengo la Shoah la kumbukizi kuhusu mauaji ya halaiki ambako elimu inatolewa kuhusu mauaji hayo.

Baraza Kuu la UN lapitisha azimio la kupinga upotoshaji na ukataaji wa mauaji ya halaiki, Guterres apongeza

Haki za binadamu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio ambalo linalaani ukataaji na upindishaji wa suala la mauaji ya halaiki au holocaust.

Azimio hilo namba A/76/L.30 limepitishwa huku kukiweko ukumbini kwa kundi la manusura wa mauaji ya halaiki yaliyofanywa na manazi wa Ujerumani dhidi ya takribani wayahudi milioni 6, idadi ambayo ni theluthi mbili ya wayahudi waliokuweko Ulaya wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Kura imepigwa siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, wakati wa mkutano wa Wansee, wakati maafisa wa ngazi ya juu wa manazi walipojadili mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi, na kuanzisha mfumo wa kambi za manazi za mauaji.

Akiwasilisha azimio hilo, Mwakilishi wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Gilad Erdan, ambaye yeye mwenyewe ni mjukuu wa manusura wa mauaji ya halaiki, amesema “dunia iko katika zama ambazo uongo unageuzwa ukweli na mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi yanasalia kuwa kumbukumbu ya mbali.”

Ameonya kuwa “hoja za kukataa kuweko kwa mauaji ya halaiki zinasambaa kama saratani na zinasambaa huku tukitazama.”

Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi.  Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.
UN / Evan Schneider
Jua likizama katika kambi ya Auschwitz-Birkenau walikopata mateso wayahudi. Kambi hii iliyopo Poland imesalia kuwa ishara ya ugaidi, mauaji ya kimbari na ya holocaust.

Guterres apongeza kupitishwa kwa azimio

Punde Baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha hatua hiyo akisema kupitishwa kwake kwa makubaliano baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, ni ishara kuwa nchi zote ambazo ni wanachama zinapaswa kulaani na kwa vitendo vidhihirishe kupinga vitendo vya kukanusha uwepo wa mauaj iya halaiki dhidi ya wayahudi.

Taarifa iliyotolewa jijini New  York, Marekani na msemaji wake imesema, “kama Katibu Mkuu anavyosema mara kwa mara, katu hatuwezi kulemaa mbele ya majaribuo ya kukanusha uwepo wa mauaji ya halaiki, kusema uongo au kupunguza makali ya kile kilichotokea. Ni lazima pia tuendane na hali ilivyo na kuchukua hatua dhidi ya mbinu mpya za chuki dhidi ya wayahudi ambayo inachochewa na nadharia zinazopangwa na pia zinazosambaa kwenye mtandao.”

Amesema Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Elimu, Sayansi na Utamaduni na program ya kuelimisha kuhusu mauaji ya halaiki, utaendelea kutekeleza program za kuelimisha zinazolenga kukabiliana na ukataaji na upotoshaji kuhusu mauaji ya kimbari.

Kikao cha Baraza Kuu la  UN hii leo 20 Januari 2022 kilipokaa na kupitisha kwa pamoja azimio la kulaani upotoshaji au ukataaji wa kuwepo kwa mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi au holocaust
Paulina Kubiak
Kikao cha Baraza Kuu la UN hii leo 20 Januari 2022 kilipokaa na kupitisha kwa pamoja azimio la kulaani upotoshaji au ukataaji wa kuwepo kwa mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi au holocaust

Azimio lenyewe

Kwa mujibu wa azimio hilo, mauaji ya halaiki yatasalia kuwa onyo kwa watu wote juu ya hatari za chuki, ubaguzi wa rangi, upendeleo na ukosefu wa stahmala.

Katika nyaraka hiyo, nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeelezea wasiwasi wao kuhusu ongezeko la matukio ya ukataaji au upotoshaji kuhusu mauaji ya halaiki unaofanywa kwa kutumia taarifa na teknolojia za mawasiliano.

Aidha linasihi nchi wanachama kukataa bila kuchelea hali yoyote ya kukataa au kupotosha mauaji ya halaiki dhidi ya wayahudi kama tukio la kihistoria.