Wanasayansi wabaini mwamba nadra wa matumbawe karibu na Tahiti

21 Januari 2022

Timu ya wanasayansi iliyokuwa imetumwa na shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni kufanya utafiti baharini imebaini moja ya miamba nadra na kubwa zaidi wa matumbawe karibu na Tahiti huko bahari ya Pasifiki.
 

Taarifa iliyotolewa na UNESCO huko Paris Ufaransa imesema mwamba huo uko katika hali nzuri kupindukia na matumbawe yana umbo la ua la waridi na ugunduzi wake ni jambo la thamani kubwa.

"Hadi leo hii, tunafahamu vyema zaidi kilichoko mwezini kuliko kilichoko chini ya bahari. Ni asilimia 20 tu ya eneo la chini ya bahari ambalo ramani yake inafahamika. Ugunduzi huu wa kipekee huko Tahiti unaonesha kazi ya kipekee ya wanasayansi ambao chini ya uratibu wa UNESCO wanapanua ufahamu wetu wa kile kilichoko chini ya miguu yetu,” amesema Audrey Azoulay, Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO.

Mwamba huo wa matumbawe uko kwenye kina cha kati ya mita 30 hadi 65 na urefu wake ni kilometa 3 katika mapana ya mita za upana 30 kwa 60, na hivyo kufanya kuwa mwamba wa matumbawe wenye hali bora zaidi na mkubwa kuwahi kurekodiwa na kufahamika duniani. Mapana ya maumbo ya waridi ya matumbawe hayo ni mita 2.

Akizungumzia ugunduzi huo, Alexis Rosenfeld ambaye ni mpiga picha kutoka Ufaransa na muasisi wa kampeni iitwayo 1 Ocean Campaign na aliongoza timu hiyo ya wanasayansi ya kupiga mbizi amesema, “Haikuwa kitu cha kawaida kuweza kuona matumbawe haya makubwa na mazuri ya rangi ya poda ambayo yametanda eneo kubwa ambalo macho yanaweza kuona. Ilikuwa kama kazi ya Sanaa.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter