Vijana lazima wawepo kwenye meza ya majadiliano ya amani- Guterres

20 Januari 2022

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amesema juhudi za vijana za kujenga na kusongesha amani bado hazijawa na mchango unaotakiwa kwa sababu hawajashirikishwa kwa kina kwenye meza ya mazungumzo.
 

Guterres amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kikao cha ngazi ya juu cha kimataifa kuhusu ujumuishaji wa vijana katika michakato ya amani, kikao kinachofanyika kwa njia ya mtandao.
Katibu Mkuu amesema katika hali hiyo ni lazima jamii ya kimataifa iongeze juhudi ili vijana washirikishwe kikamilifu na amani ya  kudumu iweze kupatikana.

“Tunahitaji kuhakikisha vijana wana kiti kwenye meza ya mazungumzo na kuweka suluhu jumuishi ambazo zinahusisha amani ana usalama, maendeleo endelevu na haki za binadamu,” amesema Katibu Mkuu.

Tupanue wigo wa uwekezaji

Guterres ameorodhesha mifano ya usaidizi wa Umoja wa Mataifa ikiwemo kupitia kamisheni za ujenzi wa amani, usaidizi ambao umepatia vijana wajenzi wa amani jukwaa la kuwasilisha kazi zao na mapendekezo yao.

Mwaka jana Mfuko wa Ujenzi wa amani ulitoa takribani dola mililnmi 26 kwa miradi ya iliyotokelezwa na wadau wa mashirika ya kiraia wanaofanya kazi kwenye maeneo ya vijana, amani na usalama.
Uwekezaji huu lazima uongezwe, amesema Katibu Mkuu, na kuwe na rasilimali zaidi ambazo vijana wanaweza kupata na kusongesha harakati zao.

Wevyn Muganda, kutoka shirika la kiraia la Haki Afrika nchini Kenya akihutubia Baraza la Usalama wakati wa mkutano  kuhusu amani na usalama hususan ajenda ya vijana na amani.(MAKTABA)
UN / Evan Schneider
Wevyn Muganda, kutoka shirika la kiraia la Haki Afrika nchini Kenya akihutubia Baraza la Usalama wakati wa mkutano kuhusu amani na usalama hususan ajenda ya vijana na amani.(MAKTABA)

Mbinu ya kujumuisha wa vijana

Huku kukiwa na ripoti ya kwamba vijana wajenzi wa amani wanakumbwa na vitisho na haki zao zinakiukwa, Katibu Mkuu ameangazia umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa haki za binadamu na fursa za kiraia ziweze kulindwa.

“Kwa minajili hiyo, Umoja wa Mataifa utatengeneza mfumo wa kufuatilia Vijana katika Siasa ambacho kitafuatilia ni kwa vipi fursa za kisiasa zimefunguliwa kwa vijana katika nchi mbalimbali, fursa ambazo vijana wanadai kwa dhahiri.”

Katibu Mkuu amepongeza vijana kwa kuzungumza wazi hasa wakati huu dunia inakabiliwa na majanga ikiwemo COVID-19, mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa mizozo na ubaguzi.

Vichocheo thabiti vya mabadiliko

Ijapokuwa vijana wameathiriwa na changamoto hizi, bado wamekuwa mstari wa mbele kuchukua hatua na kusaka majawabu.

Vijana nchini Mali wakishiriki kwenye maigizo kama njia mojawapo ya kupaza sauti ya amani.
MINUSMA/Marco Dormino.
Vijana nchini Mali wakishiriki kwenye maigizo kama njia mojawapo ya kupaza sauti ya amani.

“Nawapongeza vijana duniani kote kwa kupaza sauti zao- iwe mitaani au mtandaoni, kwa kusimama kudai hatua kwa tabianchi, usawa wa jinsia, haki kwenye masuala ya ubaguzi wa rangi na kijamii na mengine mengi,” amesema Katibu Mkuu.

Ameongesza kuwa wakati huu dunia inahaha kujikwamua kutoka janga la Corona, kuna umuhimu wa kushughulkia mzizi wa kuenguliwa kwa vijana katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

“Lazima tuwekeze katika kupatia vijana matumaini na fursa, hasa vijana wa kike ikiwemo kupitia elimu,” amesema Katibu Mkuu akiongeza kuwa vijana siyo tu raia wenye haki sawa bali pia ni mawakala thabiti wa mabadiliko ambao sauti zao lazima zisikilizwe.

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto mezani) akihutubia kikao cha ngazi ya juu kuhusu ujumuishaji vijana kwenye michakato ya amani
UN/Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto mezani) akihutubia kikao cha ngazi ya juu kuhusu ujumuishaji vijana kwenye michakato ya amani

Kusongesha ajenda

Mkutano huu wa siku mbili unaofanyika mtandao na ambao unamalizika kesho Ijumaa, umeandaliwa kwa pamoja na Qatar, Finland na Colombia.

Miongoni mwa malengo yake ni kuimarisha utashi wa kisiasa na ahadi ikiwemo za vijana kushiriki katika mikataba ya amani, na msisitizo zaidi ni vijana wa kike.

Katibu Mkuu amefurahishwa na kitendo kwamba mkutano huo kabla ya kuanza washiriki walishapitisha nyaraka mbili muhimu ikiwemo mkakati wa miaka mitano ya ujumuishaji wa vijana katika michakato ya amani.

Amewaambia washiriki yeye anashikamana nao kuhakikisha mustakabali wa dunia unakuwa jumuishi.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter