Skip to main content

Programu ya  UNRWA  yafungua macho si tu wanafunzi bali pia walimu 

Watoto katika ukanda wa Gaza
© UNRWA 2021/Mohamed Hinnawi
Watoto katika ukanda wa Gaza

Programu ya  UNRWA  yafungua macho si tu wanafunzi bali pia walimu 

Haki za binadamu

Programu ya kufundisha masuala ya haki za binadamu katika shule za watoto wakimbizi wa kipalestina katika ukanda wa Gaza,  imesaidia siyo tu wanafunzi kutambua haki zao bali pia walimu ambao wanawafundisha na hivyo kusaidia katika kusongesha amani kwenye eneo ambalo hugubikwa na migogoro.

Fatma Issa Al Hams mwalimu wa shule ya Rafah, ambayo ni shule ya maandalizi kwa wasichana, anafundisha masomo ya kijamii. Amekuwa akifanya kazi na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA kwa miaka 33 sasa. 

Anasema, “mwaka 2017 nilipata mafunzo ufundishaji wa haki za binadamu, mizozo na stahmala. Sasa ni mratibu wa Bunge la shule na kiongozi wa kamati ya shule kuhusu haki za binadamu, mizozo na stahmala.” 

Programu hii ikiungwa mkono na Marekani imekuwa ikifundishwa na UNRWA kwa miaka 20 sasa ambapo Mwalimu Fatma anasema, “kuwafundisha watoto kuhusu haki za binadamu ni muhimu kwa sababu wanapotambua haki zao wanaheshimu pia haki na wajibu wa watu wengine. Elimu ya haki za binadamu kwa watoto inaimarisha maadili yao ya stahmala, haki za watoto na pia kujiamini.” 

Na tayari mwalimu Fatma anaona mabadiliko chanya akisema, “imeimarisha kujiamini na pia kujiheshimu wao na kuheshimu wengine. Wanashiriki kikamilifu kwenye mafunzo kwa sababu wanafunzi ndio kito vu cha mchakato mzima wa masomo. Na kwangu mimi kama mwalimu, imenifungua macho kwa sababu kuna mbinu za ufundishaji ambazo awali sikuzitambua kabisa licha ya uzoefu wangu wa muda mrefu wa kufundisha.” 

Tarehe 19 mwezi Desemba mwaka 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio kuhusu elimu na mafunzo kuhusu haki za binadamu ambalo linasisitiza umuhimu wa kila mtu kuwa na haki za kufahamu, kutafuta na kupata tarifa kuhusu haki zao za binadamu na haki za aina mbalimbali za uhuru.