Mwaka 2021 watajwa miongoni mwa miaka 7 yenye joto zaidi katika rekodi:WMO
Mwaka 2021 watajwa miongoni mwa miaka 7 yenye joto zaidi katika rekodi:WMO
Shirika la hali ya hewa duniani WMO limetoa ripoti ya hali ya hewa ya mwaka 2021 na kueleza kuwa mwaka huo bado ulikuwa moja kati ya miaka saba yenye joto zaidi katika rekodi.
Ripoti hiyo ya WMO imetolewa baada ya shirika hilo kupitia kwa kina takwimu za mamlaka sita za kimataifa zinazofanya tathmini ya hali ya joto na kuonesha kuwa wastani wa halijoto duniani mwaka 2021 ilikuwa takriban nyuzi joto 1.11 °C katika kipimo cha Selsiasi.
Mwaka 2021 ni wa 7 mfululizo (2015-2021) ambapo halijoto duniani imekuwa zaidi ya nyuzi joto 1°C katika kipimo cha Selsiasi kulingana na takwimu zote za mamlaka 6 za kimataifa zilizokusanywa na WMO.
Katibu mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas amesema, “matukio yanayofuatana ya La Niña yanamaanisha kuwa ongezeko la joto la 2021 lilikuwa kidogo sana ikilinganishwa na miaka ya hivi karibuni.”
Ongezeko la joto kwa ujumla limetokana na ongezeko la gesi chafuzi ambayo sasa ni kubwa ikilinganishwa na vichochezi vya hali ya hewa vinavyotokea kiasili.
Profesa Taalas ameongeza kuwa, “mwaka 2021 utakumbukwa kwa halijoto iliyovunja rekodi ya karibu nyuzi joto 50°C nchini Canada, mvua ya kipekee, mafuriko mabaya huko Asia na Ulaya na vile vile ukame katika baadhi ya maeneo barani Afrika na Amerika Kusini. Athari za mabadiliko ya tabianchi na hatari zinazohusiana na hali ya hewa zimeleta athari mbaya kwa jamii katika kila bara moja."
Katika miaka 7 iliyopita miaka ambayo imekuwa na joto zaidi ni mwaka 2016, 2019 na 2020.